"Mauaji ya kiongozi wa Hamas sio mashambulizi kwa Lebanon" - Israel
Eric Buyanza
January 3, 2024
Share :
Israel imesisitiza kuwa mauaji ya kiongozi wa Hamas, Saleh al-Arouri huko Beirut hayakuwa mashambulizi dhidi ya Lebanon.
Msemaji wa serikali ya Israel, alisema, "Saleh al-Arouri alifariki katika shambulio dhidi ya Hamas."
Hamas imelaani mauaji hayo, huku mshirika wake Hezbollah ikisema ni shambulio dhidi ya mamlaka ya Lebanon na kuahidi kulipiza kisasi kwa mauaji hayo.
Wakati huohuo Waziri Mkuu wa Lebanon, aliishutumu Israel kwa kujaribu "kuiingiza Lebanon katika mvutano huo."
Vyombo vya habari vya Lebanon vinaripoti kwamba Arouri, naibu kiongozi wa kisiasa wa Hamas, aliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani kusini mwa Beirut pamoja na watu wengine sita - makamanda wawili wa kijeshi wa Hamas na wanachama wengine wanne.
Alikuwa kiongozi muhimu katika Brigedi za Qassam, mrengo wenye silaha wa Hamas, na mshirika wa karibu wa Ismail Haniyeh, kiongozi wa Hamas.
Alikuwa Lebanon kwa kutokana na uhusiano mzuri kati ya kundi lake na Hezbollah.
Msemaji wa Israel Mark Regev hakutaka kuthibitisha kuwa Israel ilifanya mauaji hayo, msimamo wa kawaida kwa maafisa wa Israel, lakini aliiambia MSNBC: "Yeyote aliyefanya hivyo, ni lazima ieleweke kwamba hili halikuwa shambulio dhidi ya taifa la Lebanon. Yeyote aliyefanya hivi ana uadui na Hamas. Hilo liko wazi kabisa."
Arouri mwenye umri wa miaka 57, ndiye kiongozi mkuu zaidi wa Hamas kuuawa tangu Israel ilipoingia vitani na kundi hilo baada ya shambulio la Oktoba 7.