Mbinu za Ruben Amorim kocha mpya wa Man Utd
Sisti Herman
November 9, 2024
Share :
Utangulizi
Wiki iliyopita klabu ya Manchester United imemtangaza rasmi Ruben Amorim, aliyekuwa kocha Mkuu wa Klabu ya Sporting CP ya ligi kuu nchini Ureno kuwa kocha Mkuu wa Klabu hiyo kurithi mikoba ya Erik Ten Hag waliyetangaza kuachana naye siku 5 zilizopita.
Amorim ambaye kitaaluma ana UEFA Pro License kabla ya kujiunga ametwaa Makombe akiwa na timu mbili za Ureno, Braga na Sporting CP kwenye misimu mitano tangu awe kocha;
- Primeira Liga (ligi kuu Ureno) × 2
- Taca de Liga (Kombe la ligi) × 3
- Supertaca Candido de Oliveira ×1
Je ni kocha sahihi kulingana na mahitaji ya Man Utd?
Bila shaka jibu ni ndiyo, tupo kwenye nyakati za soka ambazo kocha amepunguziwa majukumu kwa kiasi kikubwa, hata ukitazama kwenye tovuti ya klabu, namna alivyoagwa Erik Ten Hag alitamkwa kama "MANAGER" lakini ukitazama alivyokaribishwa Amorim utaona wamemtaja kama "HEAD COACH"
Utofauti wa maneno hayo unaenda kupunguza majukumu kwa Amorim, kazi yake inabaki kupandikiza mbinu kulingana na aina ya wachezaji waliopo huku usimamizi wa timu kwenye masuala ya usajili na maendeleo ulibaki kwa Viongozi wake kwenye Idara ya Ufundi kama;
- Dan Ashworth, Mkurugenzi wa michezo
- Jason Wilcox, Mkurugenzi wa Ufundi
Hao wanapunguza majukumu mengi ambayo kwa miaka iliyopita kwa Man Utd yalikuwa yakifanywa na makocha
Je Amorim anaendana na falsafa na DNA ya Man Utd?
Man Utd inasifika kwa aina ya utambulisho wake wa soka la kasi la mashambulizi ya moja kwa moja na ya kujibu huku wakizuia kwa presha kubwa huku wakitawala mchezo (Transition based team)
Lakini kwa Muongo mmoja uliopita soka limeshuhudia mabadiliko makubwa sana ya kiufundi ambapo kwasasa timu haihitaji DNA ya Falsafa zao tu kushinda bali timu zinazoshinda mechi na makombe ni zile zinazoweza kutafsiri vyema nyakati za kimbinu uwanjani, yaani;
- Mbinu bora za kushambulia (In Possession)
-Mbinu bora za kuzuia (Off Possession)
-Mbinu bora za kushambulia mashambulizi ya kujibu pindi timu inapopata umiliki wa mpira haraka (Posetive Transitions)
-Mbinu bora za kuzuia mashambulizi ya kujibu timu inapopoteza umilikiwa mpira haraka (Negative Transitions)
-Mbinu bora za mipira ya kutenga/iliyokufa (Set Plays)
Huku uchaguzi wa mbinu hizo zote kwenye michezo ukitegemea mambo mbalimbali kama;
-Ubora na udhaifu wa wapinzani (Mbinu zao, uwezo wa kiufundi wa wachezaji na utimamu wa miili)
-Aina na ubora wa kiufundi wa wachezaji waliopo kwenye kikosi
-Mazingira (hali ya hewa, uwanja n.k)
Uteuzi wa Amorim haujaja hivi hivi, ni dhahiri kuwa una mashinikizo kutokana na mahitaji ya Wakurugenzi wa Idara ya Ufundi kama Ashwoth na Wilcox, huku Afisa mtendaji mkuu Omar Berrada akiwa mmoja kati wanaovutiwa sana na kocha huyo ambaye alimhitaji sana akiwa Man City
Ni wazi kuwa uteuzi wa Amorim umeanzia kwenye michoro (Blueprint) za Ujenzi wa Man Utd mpya unaoongozwa na Ashwoth na Wilcox chini ya utawala mpya wa INEOS.
Mbinu za Amorim zipoje?
Utambulisho mbinu za Amorim
Amorim ni kocha anayependa timu yake itawale mchezo kwa kumiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga huku ikizuia kwa presha kubwa na wakiwa pamoja bila kuachina nafasi kubwa kati ya mtu na mtu pindi wasipomiliki mpira
Mfumo na staili ya uchezaji wa Amorim
Amorim ni muumini wa mfumo wa 3-4-3 ambao huwa na tabia hizi za wachezaj pale Sporting;
Kipa
Mabeki watatu wa kati (Back 3)
Viungo wawili wa kati (Double Pivot)
Viungo wawili washambuliaji (Double 10's)
Wachezaji wa pembeni wawili (Wing-Backs)
Mshambuliaji mmoja (Center Foward)
Wakimiliki mpira
Sporting CP chini ya Amorim ni timu inayopenda kutawala Mchezo wa kumiliki sana mpira wakiwa na mfumo wa 3-4-3 ambao hunyumbulika kuwa kwenye miundo tofauti kulingana na hatua za shambulizi, kama;
1. Wakijenga shambulizi kuanzia nyuma (Build up phase)
Sporting CP wamekuwa na muundo wa kipekee wakati wa kujenga shambulizi unaonyumbulika kutoka kwenye mfumo wao wa 3-4-2 na kuwa kwenye muundo wa 3-4-2-2 ambapo;
- Mabeki wawili wa kati wa pembeni huungana na kipa kuwa watatu nyuma
- Beki wa kati husogea usawa wa kiungo wa kati, sambamba na wachezaji wa pembeni, na kuwa wanne kwenye mstari wa pili wa Ujenzi wa shambulizi
- Kiungo wa kati mmoja husogea usawa wa kiungo mshambuliaji, na kiungo mshambuliaji mmoja husogea usawa wa mashambulizi kukamilisha umbo la 3-4-2-2
Lengo la Sporting CP kujenga mashambulizi kuanzia nyuma ni kuhamasisha wapinzani kuwafuata kwao ili kutengeneza nafasi/mianya katikati ya mistari yao ya uzuiaji pindi wanapowafuata au nyuma Kisha Sporting CP kujenga shambulizi la pasi fupi katikati ya mianya hiyo wakitegemea faida hizi;
- Idadi (Numerical Superiority) kwenye kila eneo, mfano kwenye.mstari wa kwanza wa Ujenzi wa shambulizi Sporting CP ina wachezaji watatu dhidi ya wapinzani, na wengine wanne wanaoweza kuendeleza shambulizi kwa njia za katikati (Central Progressions) wachezaji wawili wa kati au njia za pembeni (Wide Progressions) kwa wawili wa pembeni
- Uwezo (Qualitative Superiority), Faida kubwa waliyonayo wachezaji wa Sporting CP wanaojenga shambulizi kuanzia nyuma ni uwezo wao wa kiufundi wa kupiga pasi hasa wanapokuwa kwenye shinikizo kubwa la wapinzani, wanaweza kutoka under pressure
Hizi ni njia 3 za build up za Sporting CP baada ya ku-attract Pressure;
- Kupita katikati kwa mawasiliano kati ya watatu wa nyuma na wawili wa kati kwenye mstari wa pili wa Ujenzi wa shambulizi (Passing through the Press)
- Kupita pembeni kwa mawasiliano kati ya watatu wa nyuma na wawili wa pembeni kwenye mstari wa pili wa Ujenzi wa shambulizi (Passing around the Press)
- Kupita juu kwa kulenga wachezaji wa mbele au nafasi nyuma ya ukuta wa wapinzani wanao-press na highline (Passing Over the Press)
2. Theluthi ya katikati na mbele (Middle and Final Third)
Wakiwa kwenye theluthi mbili za mbele Sporting CP huwa kwenye umbo la 3-4-3 lenye umbo la box katikati (3-box-3) ambapo;
- Mabeki watatu wa nyuma
- Viungo wawili wa kati mbele yao
- Viungo washambuliaji wa kati
- Wachezaji watatu kwenye mstari wa mwisho, mshambuliaji na wachezaji wa pembeni
Mgawanyo wa majukumu huwa hivi;
(I) Back 3; Watatu wa nyuma ambao ni mabeki wa kati huwa na jukumu kubwa la kutawala possession na kuweza kujenga na kuendeleza shambulizi kwa njia mbili;
- katikati, kwa viungo wawili wa Katikati wanaokuwa nyuma ya mstari wa kwanza wa ulinzi wa wapinzani
- Pembeni wa wachezaji wa pembeni kwenye Mapana ya uwanja
(II) Progressions; Uendelzwaji wa shambulizi huweza kutokea kwa kwa mawasiliano kati ya viungo wa kati na Viungo washambuliaji ambao huwa nyuma ya mstari wa pili wa ulinzi wa timu pinzani
(II) Penetrations; upenyaji wa kuta za uzuiaji za wapinzani hutegemea namna wachezaji wa pembeni wanavyoshawishi kuta za wapinzani kutanua pembeni na kuacha mianya ambayo viungo washambuliaji wa kati huji-position na kupokea mipira Kisha kuendelea kwenye mbele
(III) Creation; Utengenezaji wa nafasi hutegemea zaidi pasi mpenyezo za viungo washambuliaji, link up play za mshambuliaji na wachezaji wa pembeni kupiga krosi baada ya Kukosekana mianya katikati ya Kuta za wapinzani
(IV) Finishing; humtegemea zaidi mshambuliaji mmoja wa kati ambaye huwa na uwezo mkubwa wa kubadili nafasi zinazotengenezwa kuwa mabao, mzuri kwenye kufunga mipira ya juu, mzuri kushambulia nafasi nyuma ya mabeki
Kwasababu mara nyingi Sporting CP wanapenda kutawala umiliki wa mpira, nyakati nyingi wapinzani wanaocheza nao huwa wengi nyuma ya mpira kiasi kwamba kuna nyakati kutokana na wingi wao Sporting CP hushindwa kuwa wafanisi kumiliki mpira na kuvunja mistari yao ya uzuiaji na kupoteza umiliki wa mpira hivyo kuwa kwenye hatari ya kufanyiwa mashambulizi ya kujibu kabla hawajarejea kwenye muundo wao wa uzuiaji (Counter Attacks)
Sporting CP kuepuka hali hii wamekuwa bora sana kuanza kuzuia kuanzia wanapopoteza mpira (Counter Pressing) huku wakiwa na umbo bora linaloweza kumeza mashambulizi ya kujibu (rest defence)
Wasipomiliki mpira
Sporting CP huanza kuzuia kuanzia kwenye theluthi ya kwanza ya Ujenzi wa shambulizi ya wapinzani wakiwa na muundo wa 5-2-3 ambao kuna nyakati hubadilika na kuwa kwenye miundo mingine kama 3-4-3 kwa kutegemea na namna wapinzani wao wanavuofanya Build up huku wao wakijitahidi ku-adapt idadi ya wachezaji wanaoweza kuendeleza shambulizi
Wakizuia kuanzia mbele (High Press)
- Mshambuliaji mmoja ana-press kipa na mabeki
- Nyuma yake, viungo washambuliaji huwa dhidi ya viungo wa kati wa wapinzani wanaoweza kuendeleza shambulizi
- Pembeni yake, Wachezaji wa pembeni huwa dhidi ya mabeki wa pembeni wa wapinzani wanaoweza kuendeleza shambulizi
Nia ya kuzuia kwa presha kubwa, pamoja kuanzia mbele ni kuweza kuwalazimisha wapinzani kukosea na wao kupora mpira ili kufanya shambulizi la kujibu kabla wapinzani hawajarudi kwenye muundo wao wa ulinzi (Positive transitions)
Wakiwa wanazuia kwenye theluthi mbili za nyuma (Mid & Low Block)
Sporting CP huzuia na umbo la 5-2-3 wakiwa pamoja, wameufinya uwanja bila kuachiana nafasi huku wakiwa wamezuia njia za wapinzani Kupita kama;
1. Katikati, wachezaji watatu wa mbele huzuia mabeki wa wapinzani kuwa huru na mpira na kuwasiliana na viungo katikati ya mistari, huku viungo wa kati mbele ya mabeki wakizuia viungo washambuliaji wa wapinzani kuwa huru katikati ya mistari
2. Pembeni, wachezaji wa pembeni huzuia mabeki wa pembeni wa wapinzani kuwavuta pembeni mabeki wao wa kati na kutanua ukuta wao kutengeneza mianya
3. Juu, mabeki wa kati huzua washambuliaji wa timu pinzani kuwa huru kwenye mipira ya juu na ya chini
Kwenye staili hii Sporting CP imekuwa haifikiki kirahisi langoni mwao
Viini muhimu kwenye mbinu za Amorim
Kama ilivyo kwa makocha wengi wenye utambulisho wa mbinu zao za uchezaji, Ruben Amorim pia ana mambo ambayo hutambulisha mbinu za uchezaji za timu yake ambazo hubeba mizizi na kiini cha ubora wa utambulisho wake.
1. Box Midfield
- Amorim kama ilivyo kwa makocha wengi wa daraja la juu hivi sasa yeye pia hutumia viungo wanne wa kati ambao kimuundo hutengeneza umbo la sanduku (Box Midfield) kwenye muundo wa 3-4-2-1.
• Viungo wawili wa chini mbele ya mabeki watatu (double pivot)
• Viungo wawili washambuliaji nyuma ya mshambuliaji wa kati (double 10's)
- Viungo hawa huwa na majukumu ya kusaidia kazi ya kuendeleza mashambulizi yanayojengwa kuanzia nyuma, kupenya kuta za wazuiaji na Kutengeneza nafasi
• Double Pivot, viungo wawili wa kati ambao hucheza kati ya mstari wa kwanza na wa pili wa uzuiaji wa wapinzani hupokea pasi kutoka kwa mabeki watatu na kuendeleza shambulizi kwa njia ya Kati au pembeni
• Double 10's, viungo wawili washambuliaji ambao hucheza nyuma ya viungo wa wapinzani hupokea shambulizi na kusaidia timu kupenya na Kutengeneza nafasi hasa kwa njia za kati
2. Wing-backs
- Amorim pia anatumia wachezaji wa pembeni (Wing-Backs) kama kiini cha mbinu zake kwenye muundo wa 3-4-2-1 ambao kuna muda huwa kwenye umbo la 3-box-3
- Wachezaji hao wa pembeni hushiriki majukumu mbalimbali kama;
• Kuzuia njia za pembeni kwenye mstari wa mabeki pindi timu ya inapozuia, wakiwa kwenye muundo wa 5-2-3
• Kuendeleza mashambulizi kwa njia za pembeni wao wakiwa kama Viungo wa pembeni kwenye muundo wa 3-4-3
• Kusaidia timu ya kupenya kupitia njia za pembeni na Kutengeneza nafasi wakiwa kwenye nusu ya mpinzani kwenye muundo wa 3-2-4-1
3. Rest Defence
- Sporting CP ni timu inayopenda kuwa na utawala wa mpira nyakati zote, hivyo humiliki mpira sana, na kutanua uwanja ili kurahisisha kufungua wapinzani
- Katika hali hiyo ni rahisi sana kwa wapinzani kuwashambulia kwa mashambulizi ya kujibu (Counter attacks) pindi wanapopokonya mpira na kuwashambulia Sporting CP kwa haraka kabla hawajarejea Muundo wao wa uzuiaji
- Kwa kupunguza madhara Kutokana na athari hizo, Amorim akatengeneza mbinu zenye muundo wenye uwiano mzuri wa kuzuia Counter attacks ambapo huwa na wachezaji watano wanaposhambulia na watano wanaoweza kuzuia Counter attacks, yaani Wakati;
• Wing-backs, double 10's na mshambuliaji wapo kwenye theluthi ya mwisho ya wapinzani kwaajili ya kupenya, Kutengeneza nafasi na kufunga
• Double Pivot na Back 3 wapo kwenye muundo mzuri kuzuia mashambulizi ya kujibu endapo wachezaji wa mbele watapoteza mpira
- Muundo huo huwa na Layer mbili zinazotengeneza muundo wa 3+2;
• Nyuma wanakuwa mabeki wa Kati (Back 3)
• Mbele yao huwepo Viungo wawili wa kati ambao hawahamihami kwenye nafasi zao
- Muundo huu humeza na kuzima Counter attacks za wapinzani wao