Mbinu za Xabi Alonso zilizotawala 2023-24
Sisti Herman
April 15, 2024
Share :
Utangulizi
Kocha Xabi Alonso ameiongoza Bayer Leverkusen kwenye michezo 43 ya mashindano yote msimu huu wa 2023/24 hadi sasa bila kupoteza (unbeaten), huku wakiwa;
• Mabingwa wa ligi kuu Ujerumani (Bundesliga) wakiwa na mechi 5 mkononi
• Wamefika hatua ya fainali ya kombe la ligi (DFB Pokal)
• Wamefika robo fainali ya Europa league
- Ikumbukwe kocha huyo ambaye ni mchezaji wa zamani wa Real Madrid, Liverpool na Bayern Munich aliichukua Leverkusen ikiwa nafasi ya pili kutoka mwisho kwenye Bundesliga msimu wa 2022/23 ikiwa Katikati ya msimu na kuifanikisha kumaliza nafasi ya 6.
- Kabla ya hapo Alonso alianzia ufundishaji kwenye timu za vijana za Real Madrid na Real Sociedad baada ya kustaafu soka
Mbinu
Xabi ni kocha anayeamini kwenye mbinu za kuutawala mchezo kwa nyakati zote kuwa na umiliki wa mpira na kuutunza kwa pasi fupi za haraka na uhakika, kutengeneza nafasi na kufunga huku wakizuia kwa presha kubwa kwa wapinzani ili kuwalazimisha wakosee.
- Wachezaji ambao amewatumia sana kwenye kikosi chake ni;
• Lucas Hradecky (GK)
• Odilon Kassounou (RCB)
• Jonathan Tah (CCB)
• Edmond Taqsoba (LCB)
• Granit Xhaka (CM)
• Exequel Palacios (CM)
• Alejandro Grimaldo (LWB)
• Jeremie Frimpong (RWB)
• Florian Wirtz (RAM)
• Jonas Hoffman (LAM)
Victor Boniphace (CF)
Hizi hapa mbinu za Xabi;
Wakizuia
- Wasipokuwa na umiliki wa mpira Beyer Leverkusen huzuia kwa idadi kubwa nyuma ya mpira, kwa shinikizo kubwa kwa wapinzani kwenye kila theluthi ya uwanja
- Muundo wa uzuiaji wa Leverkusen huwa kwenye mfumo wa 5-4-1, ambapo;
• Mstari wa kwanza wa uzuiaji huwa na mshambuliaji mmoja Victor Boniphace
• Mstari wa pili wa uzuiaji huwa na viungo wanne, Xhaka & Palacious (Kati) na Hoffman & Wirtz (pembeni)
• Mstari wa nyuma wa uzuiaji huwa na mabeki watano, Taqsoba, Tah & Kassounou (Kati) na Grimaldo & Frimpog (pembeni)
- Pindi Leverkusen wanapozuia kwenye nusu ya mpinzani, Muundo wa 5-4-1 hautoi idadi nzuri ya wazuiaji kwenye mstari wa mbele (Pressing Structure) dhidi ya safu ya wapinzani wanaojenga shambulizi kuanzia nyuma (Build Structure), kwani Mshambuliaji huwa dhidi ya Zaidi ya wachezaji watatu wa Leverkusen hivyo huwa rahisi kuvukwa kwa faida ya idadi (Numerical Superiority)
- Lakini Leverkusen hutumia mbinu mbili wanapozuia ili kumeza mapungufu hayo ya kimuundo;
1. Mtego (Pressing trap); Mshambuliaji wa Leverkusen anavyoenda kushinikiza wapinzani wanapojenga shambulizi, hulazimisha wapite pembeni huku akiwa amezuia njia ya mabeki na kipa wa wapinzani kuweza kumpa pasi kiungo wa kati ili kuendeleza shambulizi, wapinzani hulazimika kupita juu au pembeni
2. Kichocheo (Pressing trigger); Baada ya kutega mtego na mpinzani kunasa kwenye mtego wao, Leverkusen hutumia njia hizo mbili kama kichocheo cha wao kushinikiza kwa nguvu na kasi Zaidi;
• Kama wapinzani wakipita juu, Leverkusen huhakikisha wanashinda mipira ya juu na inayodondoka
• Kama wapinzani wakipita njia za pembeni (hasa kwa Full-backs) Leverkusen hushinikiza upand huo kwa idadi kubwa zaidi na kuwabana wapinzani kwenye eneo dogo
- Kwenye trigger hiyo, wapinzani wakipita pambeni Leverkusen huzuia nafasi (Zonal marking) na wapinzani mmoja mmoja (Man marking) wanaoweza kuendeleza shambulizi lililojengwa kwa;
• Victor Boniphace huzuia njia ya pasi kurudi beki wa kati au kipa
• Viungo wa kati, Xhaka & Palacious huzuia Viungo wa Kati wa wapinzani wasiwe huru kupokea na kuendeleza shambulizi
• Viungo washambuliaji wa pembeni, Hoffman & Wirtz huzuia mabeki wa pembeni( mmoja mwenye mpira) kushindwa kuwasiliana na viungo wa pembeni
- Pindi Leverkusen wanapozuia kwenye nusu yao, hubana zaidi nafasi kwa kuufinya uwanja kwenye kina na mapana (Compactness) huku muundo wao wa 5-4-1 ukizuia njia za wapinzani kupenya kuta zao kwa presha kubwa kwenye mpira;
• Boniphace mbele huzuia kiungo mzuiaji au mabeki wa Kati wa wapinzani kuwa huru kuchezesha timu
• Xhaka na Palacios huzuia Viungo washambuliaji wa wapinzani kuweza kupenya na Kutawala njia za kati kwa kulinda nafasi mbele ya mabeki wa Kati na Kutoruhusu utawala wa wapinzani Katikati ya mistari
• Wirtz na Hoffman huzuia mabeki wa pembeni wa wapinzani kutoweza kushambulia mapana ya uwanja na Kutengeneza hali ya wawili dhidi ya mmoja (2v1) kwa mabeki wao wa pembeni Grimaldo na Frimpog ambao huwazuia washambuliaji wa wapinzani kwenye mapana ya uwanja
• Mabeki wa Kati, Taqsoba, Tah & Kassounou huhakikisha washambuliaji wa wapinzani hawashindi mpira wowote wa kugombania, juu au chini, huku viungo wao wakiokota mali
- Baada ya kuzuia njia hizo, Leverkusen pia huamini kwenye kushambulia nafasi inayoachwa nyuma na wapinzani pindi wabapopokonya mpira (Positive Transitions) ambapo hujibu mashambulizi (Counter attacks) kwa;
• Uharaka
• Idadi kubwa kwenye nafasi hizo
• Ufanisi mkubwa wa matendo (kukokota, pasi, mikimbio na umaliziaji)
Wakishambulia
Bayer Leverkusen ni timu inayopenda kutawala kwa kumiliki mpira uwanjani, kujaribu kupenya na Kutengeneza nafasi za kufunga kwa wapinzani kwa kuwalazimisha huku wakitumia muundo wa 3-4-2-1 ambapo hubadilika kulingana na hatua za kushambulia mpinzani, kama;
• Wakiwa kwenye theluthi ya kwanza na ya kati 3-4-2-1 ambapo hufanya ujenzi, Uendelezaji wa shambulizi
• Wakiwa kwenye theluthi ya mwisho 3-2-4-1 ambapo hufanya upenyaji wa Kuta za wazuiaji, utengenezaji na umaliziaji wa nafasi
1. Ujenzi wa shambulizi kuanzia nyuma (build up)
- Wakiwa kwenye theluthi ya kwanza ya uwanja kutoka kwako, Leverkusen hujenga shambulizi kwa kutumia watu wanne, kipa Lukas Hradecky na mabeki watatu wa kati ambao hutengeneza miundo tofauti kuanzia nyuma kama;
• 1-3, kipa huwa nyuma ya mabeki watatu, hutumia muundo huu wapinzani wakizuia kwa shinikizo dogo na idadi ndogo
• 4, kipa huwa Sambamba/Katikati ya mabeki watatu Kutengeneza muundo wa watu wanne ili kufaidika na idadi kubwa (Numerical Superiority) kwenye mstari wa nyuma wa ujenzi wa shambulizi dhidi wapinzani wanaozuia Kwa shinikizo kuanzia mbele
- Ujenzi wa shambulizi kuanzia nyuma hufanikiwa vyema Kutokana na namna mstari wa pili unavyotengeneza mazingira rafiki ya kupokea na kuendeleza shambulizi hasa mabeki na kipa wanapokuwa under pressure
2. Uendelezaji wa shambulizi (progression)
- Uendelezaji wa shambulizi lililojengwa kuanzia nyuma hutegemea njia 2;
• Njia ya Kati, kupitia kwa viungo wawili wa kati Xhaka & Palacious (double pivot)
• Njia ya pembeni, kupitia kwa watu wa pembeni Grimaldo & Frimpog (Wing-backs)
- Kwenye muundo wao wa 3-4-2-1, Leverkusen hutumia watu wanne wa mstari wa pili kuendeleza shambulizi linalojengwa kuanzia nyuma
- Hutumia njia ya Kati kwa Xhaka na Palacios kuendeleza shambulizi Kwa kutumia pasi za mbele na haraka zinazovunja mistari na kuwatafuta Viungo washambuliaji wawili Wirtz na Hoffman wanaokuwa nyuma ya mstari wa Viungo wa timu pinzani
- Kama wapinzani watazuia vizuri njia za kati kwa kuwa na nidhamu nzuri ya kuzuia nafasi za Xhaka na Palacious kuwasiliana na Wirtz na Hoffman, Leverkusen huchagua njia za pembeni kupitia kwa Grimaldo na Frimpog wanaocheza kwenye mapana ya uwanja kuendeleza shambulizi
3. Kupenya kuta za wazuiaji (penetrations)
- Pindi wanapoanza kuvuka mstari wa Katikati, nusu ya wapinzani, Leverkusen hutumia namna tofauti kuweza kupenya kuta za wapinzani wao, mfano;
• Kutengeneza pembetatu za pembeni (wide triangles)
• Wachezaji Kubadilishana nafasi uwanjani (Players positional rotations)
• Kuongeza idadi eneo lenye presha (Overloads)
- Leverkusen hutengeneza pembetatu muhimu maeneo ya pembeni mwa uwanja ili kufungua njia za kupenya kuta za wapinzani wanaokuwa wengi kwenye nusu yao, ambapo;
• Wing-backs, Grimaldo na Frimpog hutanua kwenye mapana ya uwanja, ili kuwavuta wazuiaji pembeni
• Viungo washambuliaji wawili, Wirtz na Hofmann kushambulia nafasi zinazojitokeza katikati ya mistari baada ya wachezaji wa pembeni wa wapinzani kuwafuata Wing-backs wa Leverkusen
• Double Pivot, Palacios na Xhaka huwa na jukumu la kukamilisha muundo wa triangles hizo ambapo jukumu lao ni kusapoti shambulizi kwa kuwachezesha Wing-backs na namba 10 wiwili
- Leverkusen pia wawapo uwanjani, wachezaji wao hubadilishana nafasi ili kuwavuruga wapinzani kwenye miundo yao ya uzuiaji hasa wanapo-mark mchezaji kwa mchezaji, kuhamahama huwafanya kuwaondoa wapinzani kwenye nafasi zao (dragging out of positions) na kuvuruga miundo yao, mfano;
• Wing-backs na viungo washambuliaji hubadilishana sana nafasi
• Double Pivot na Center Backs hubadilishana sana nafasi
• Mshambuliaji kubadilishana nafasi na Wing-backs au Viungo washambuliaji
- Pia, Leverkusen huwa na tabia ya mchezaji mmoja kuongezeka eneo ambalo limezidiwa idadi na wapinzani ili kusaidia kutoka kwenye presha na kupenya, mfano;
• Victor Boniface husogea hadi kwenye katikati ya mistari ili kusaidia timu kupenya kwenye njia za katikati, au husogea kwenye maeneo ya pembeni ya uwanja (Wide Overloads)
• Kuna nyakati Center Backs husogea hadi pembeni kuongeza idadi au husogea katikati ya mistari
4. Utengenezaji na umaliziaji wa nafasi (Creations na finishing of Chances)
- Baada ya kupenya kuta za wazuiaji, kazi inayobakia huwa utengenezaji wa nafasi ambapo Leverkusen hutengeneza nafasi kutokea maeneo tofauti;
• Krosi na Cutback passes za wachezaji wa pembeni
• Pasi mpenyezo kutoka kwa viungo wa kati
• Pasi ndefu kutoka nyuma zinazoelekezwa nyuma ya mstari wa mabeki wa wa wapinzani
- Umaliziaji wa nafasi wa Leverkusen hutegemea Zaidi;
• Mikimbio na namna mshambuliaji wao wa Kati anavyojiweka kwenye maeneo sahihi kwenye theluthi ya mwisho ya uwanja (Positioning and Movements) ambazo huhusiana na Mbinu za timu
• Idadi kubwa ya wachezaji kwenye box la wapinzani, kuna nyakati wachezaji wa Leverkusen huwa Zaidi ya 6 kwenye box
- Kutokana na kutumia muundo wa 3-4-2-1, muundo huu pia huwasaidia Leverkusen kuzuia mashambulizi ya kujibu ya wapinzani pale wanapopoteza mpira kwenye nusu ya wapinzani, kwani hutengeneza muundo rafiki kwenye mistari miwili ya nyuma, ambapo;
• Wachezaji watano hushambulia kwa wapinzani yaani mshambuliaji (usawa wa mabeki wa wapinzani), Viungo washambuliaji wawili (half Space) na Wing-backs wawili (flanks)
• Wachezaji watano huwa kwenye mistari miwili ya nyuma yaani, Layer ya kwanza ina mabeki watatu wa kati na Layer ya pili ina Viungo wawili wa kati mbele yao
- Layer hizi mbili hutengeneza muundo ambao husaidia timu kupokonya mashambulizi ya kujibu pindi wachezaji wa mbele wanapopoteza mpira na kushindwa kuwazuia (Counter Press) wapinzani kushambulia kabla Leverkusen hawajajipanga kuzuia (Negative Transitions)
Viini muhimu vya mbinu za Alonso
1. Box Midfield
- Xabi Alonso kama ilivyo kwa makocha wengi wa daraja la juu hivi sasa yeye pia hutumia viungo wanne wa kati ambao kimuundo hutengeneza umbo la sanduku (Box Midfield) kwenye muundo wa 3-4-2-1.
• Viungo wawili wa chini mbele ya mabeki watatu (double pivot)
• Viungo wawili washambuliaji nyuma ya mshambuliaji wa kati (double 10's)
- Viungo hawa huwa na majukumu ya kusaidia kazi ya kuendeleza mashambulizi yanayojengwa kuanzia nyuma, kupenya kuta za wazuiaji na Kutengeneza nafasi
- Majukumu hayo ya kimbinu huunganisha theluthi tatu za uwanja ambapo;
• Double Pivot, Xhaka na Palacious ambao hucheza kati ya mstari wa kwanza na wa pili wa uzuiaji wa wapinzani hupokea pasi kutoka kwa mabeki watatu na kuendeleza shambulizi kwa njia ya Kati
• Double 10's, Wirtz na Hoffman ambao hucheza nyuma ya viungo wa wapinzani hupokea shambulizi na kusaidia timu kupenya na Kutengeneza nafasi hasa kwa njia za kati
2. Wing-backs
- Xabi pia anatumia wachezaji wa pembeni Grimaldo na Frimpong kama kiini cha mbinu zake kwenye muundo wa 3-4-2-1
- Wachezaji hao wa pembeni hushiriki majukumu mbalimbali kama;
• Kuzuia njia za pembeni kwenye mstari wa mabeki pindi timu ya inapozuia, wakiwa kwenye muundo wa 5-2-3
• Kuendeleza mashambulizi kwa njia za pembeni wao wakiwa kama Viungo wa pembeni kwenye muundo wa 3-4-3
• Kusaidia timu ya kupenya kupitia njia za pembeni na Kutengeneza nafasi wakiwa kwenye nusu ya mpinzani kwenye muundo wa 3-2-4-1
3. Rest Defence
- Bayer Leverkusen ni timu inayopenda kuwa na utawala wa mpira nyakati zote, hivyo humiliki mpira sana, na kutanua uwanja ili kurahisisha kufungua wapinzani
- Katika hali hiyo ni rahisi sana kwa wapinzani kuwashambulia kwa mashambulizi ya kujibu (Counter attacks) pindi wanapopokonya mpira na kuwashambulia Leverkusen kwa haraka kabla Leverkusen hawajarejea Muundo wao wa uzuiaji
- Kwa kupunguza madhara Kutokana na athari hizo, Xabi akatengeneza mbinu zenye muundo wenye uwiano mzuri wa kuzuia Counter attacks ambapo huwa na wachezaji watano wanaposhambulia na watano wanaoweza kuzuia Counter attacks, yaani Wakati;
• Wing-backs, double 10's na mshambuliaji wapo kwenye theluthi ya mwisho ya wapinzani kwaajili ya kupenya, Kutengeneza nafasi na kufunga
• Double Pivot na Back 3 wapo kwenye muundo mzuri kuzuia mashambulizi ya kujibu endapo wachezaji wa mbele watapoteza mpira
- Muundo huo huwa na Layer mbili zinazotengeneza muundo wa 3+2;
• Nyuma wanakuwa mabeki wawili wa Kati Tah, Kassounou na Taqsoba (Back 3)
• Mbele yao huwepo Viungo wawili wa kati, Xhaka na Palacious ambao hawahamihami
- Muundo huu humeza na kuzima Counter attacks za wapinzani wao