Mbwa atafuna milioni 10 za bosi wake
Eric Buyanza
January 5, 2024
Share :
Mbwa anayeitwa Cecil, wa huko Pennsylvania nchini Marekani, amepata umaarufu wa ghafla kila kona ya dunia baada ya kutafuna bahasha ya pesa ambayo wamiliki wake walikuwa wametenga kwa ajili ya kumlipa fundi ujenzi.
Mabosi wa mbwa huyo waliofahamika kwa majina ya Clayton na Carrie waliweka bahasha iliyokuwa na $4,000 (milioni 10 za kibongo) kwenye kabati la jikoni kwa ajili ya kumlipa fundi aliyekuwa akiweka uzio wa nyumba yao.
Dakika 30 baadaye, kwa mshangao, walimkuta mbwa wao huyo kipenzi akifurahia mlo wa thamani zaidi maishani mwake, akiacha vipande vichafu vya pesa vilivyotawanyika kila kona ya nyumba.
"Ghafla Clayton alifoka kwa sauti, 'Cecil anakula $4,000!'" Carrie Law alisema katika mahojiano na gazeti la Pittsburgh City Paper. "Nilifikiri, 'Sijasikia vizuri.' Nilisogea na kupata mshtuko wa moyo."
Carrie Law anasema mbwa huyo...."Yupo tofauti unaweza kuacha nyama kwenye meza, na asiiguse kwa sababu yeye si mpenzi wa chakula,"....."Lakini inaonekana anapenda pesa."
Baada ya tukio hilo iliwapasa wanandoa hao Clayton na Carrie kuanza kibarua cha kuunganisha pesa zilizochanika...kazi ambayo hawakuitarajia.