Mchungaji aeleza anavyopigwa na mkewe
Eric Buyanza
December 14, 2023
Share :
Huko nchini Kenya, mchungaji mmoja wa Kanisa la kiroho ametoa kali ya mwaka baada ya kuweka wazi kuwa huwa anachezea kichapo kutoka kwa mkewe kila anapofika nyumbani.
Mchungaji huyo anasema mkewe amekuwa akimchapa na hata kumsababishia majeraha kwenye sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kwa mujibu wa chanzo chetu (Taifa Leo), mke huyo amemgeuza mumewe kama mtoto aliyeshindikana anayestahili kurekebishwa kwa mijeledi.
Pamoja na kipigo anachopokea mchungaji ameshindwa kumuacha mwanamke huyo.
“Imani yangu hainiruhusu kumpiga au kuondoka kwenye ndoa ambayo imepangwa na Mungu. Ndio, naumia na iwapo nitamlipizia kipigo anachonipiga, ukweli ni kuwa ataumia, vita vyangu ni vya kiroho na sio sehemu za mwili,” anasema mchungaji huyo.
Mchungaji huyo ambaye ana waumini wengi kwenye kanisa lake, anasema imefikia mahali anashindwa hata kutoa ushauri kwa waumini wake wenye shida kwenye ndoa zao kutokana na matukio anayopitia yeye binafsi.
“Wakati huu napitia wakati mgumu kusuluhisha vita vya wanandoa, hakuna anayejua naumizwa na mke wangu, nakuwa na moyo mgumu kuwaelekeza kwa sababu hata mimi kwangu hali si hali,” alifafanua mchungaji huyo.