pmbet

Mei 2026 imeacha alama kwenye 'Diary' za Fiesal, Chama na Okello

Sisti Herman

August 17, 2026
Share :

Utangulizi

Mwezi Mei 2026, unaweza kuwa mwezi bora zaidi kwenye msimu huu kwa wachezaji watatu nyota wa Ligi kuu ya NBC (NBC Premier League) Feisal Salum wa Azam FC, Clatous Chama wa Simba SC na Allan Okello wa Yanga SC ambao wameonyesha kiwango cha juu kwenye mwendelezo bora kwa mwezi mzima.

 

Wametikisa Takwimu za Ligi.

 

Kati ya jumla ya magoli 121 yaliyofungwa kwenye mechi 45 za Ligi kuu ya NBC ndani ya mwezi huo, Magoli 27 yamechangiwa na nyota hao ambapo;

 

1. Feisal Salum (Azam FC)

 - Goli - 7

 - Asisti - 1

 

2. Clatous Chama (Simba SC)

 - Goli - 5

 - Asisti - 4

 

3. Allan Okello

 - Goli - 9

 - Asisti - 1

 

Wanatumiwa vipi Kimbinu?

 

Wachezaji hao wote watatu kwa pamoja hutumiwa kama viungo washambuliaji wa kati, nyuma ya mshambuliaji wa mwisho kwenye mifumo ya uchezaji inayofanana, ambapo;

 

Feisal, kwenye mbinu za Florent Ibenge pale Azam FC mara nyingi hucheza nyuma ya Kitambala Bola kwenye mfumo wa 4-2-3-1, ambapo wakati wa kuzuia huwa usawa wa mshambuliaji huyo raia wa Congo DR kwenye muundo wa 4-4-2.

 



Okello, kwenye mbinu za Abdihamid Moallin pale Yanga SC mara nyingi hucheza nyuma ya Prince Dube kwenye mfumo wa 4-2-3-1, ambapo wakati wa kuzuia huwa usawa wa mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe kwenye muundo wa 4-4-2.

 

 

Chama, kwenye mbinu za Steve Berker pale Simba SC mara nyingi hucheza nyuma ya Ellie Mpanzu kwenye mfumo wa 4-2-3-1, ambapo wakati wa kuzuia huwa usawa wa mshambuliaji huyo raia wa Congo DR kwenye muundo wa 4-4-2.

Namna walivyozipa timu zao Magoli na Asisti

 

Makala hii inaonyesha namna ambavyo uwezo wa kiufundi na uelewa wa kimbinu wa wachezaji hawa umeweza kuwa mwiba mkali kwa wapinzani wao kiasi cha kuweza kuweka historia hizo;

 

Feisal Salum

 

Feisal ameonysha hatari zaidi wakati wa mipira ya kutenga (Set Pieces) ambapo kati ya magoli 8 aliyochangia Feisal kwa mwezi Mei (Goli 7 na Asisti 1), magoli mawili (dhidi ya Mtibwa Sugar na Pamba Jiji) yametokana na ubora wake wa kushambulia nafasi kwenye boxi wakati wa kona na kufunga kwa kichwa huku magoli mengine mawili akifunga kwa mikwaju ya penalti)

 

 

Pia Feisal ameonyesha ubora kwenye upishi na umaliziaji wa kiwango cha juu kwenye mipira ya krosi wakati timu yake ikiwa na mpira (In Possession) kwenye eneo la mwisho la wapinzani ambapo ameweza kutoa asisti ya goli dhidi ya Mtibwa Sugar kwa krosi kali huku yeye pia akifunga kwa kichwa akimalizia krosi kwenye mchezo dhidi ya KMC.

 

 

 

Kwenye mashambulizi ya kujibu pindi Azam FC inapopora mpira (Positive Transitions) Feisal ameonekana kuwa silaha muhimu kushambulia nafasi nyuma ya washambuliaji wake ambao hupokea mipira kutoka nyuma wakiwa kwenye shinikizo la wapinzani na kutengeneza nafasi kwake, mfano ni goli dhidi ya KMC.

 

 

 

 

 

Allan Okello

 

Kati ya magoli 10 aliyochangia kwa mwezi Mei, Okello amefunga goli 5 na kutoa asisti ya goli moja pindi Yanga inapokuwa na mpira (In Possession) ambapo amekuwa hatari kushambulia nafasi nyuma ya viungo wa timu pinzani nje ya boxi (Zone 14) mfano mchezo dhidi ya KMC na Coastal Union na hata Singida aliweza kufunga kutoka eneo hilo kwa mpira wa madhambi (Set Play hasa Freekick).

 

 

 

 

Pia nyota huyo amekuwa hatari kushambulia kwenye nafasi kati ya walinzi wa kati na wa pembeni (Half Spaces) mfano kwenye mechi dhidi ya Coastal Union ambapo alitoa asisti kwa Max kutoka kwenye eneo hilo



Mara zingine nafasi nyuma ya walinzi hasa kwenye mashambulizi ya kujibu pindi Yanga inapopora mpira na kushambulia kabla wapinzani wao hawajarejea kwenye muundo wao mzuri wa kuzuia (Positive Transitions) mfano kwenye mechi dhidi ya Dodoma Jiji.

 

 

 

 

Clatous Chama

Kati ya magoli 9 aliyochangia kwenye mwezi Mei, Magoli 6 ya Chama yametokea wakati wa mashambulizi ya kujibu (Positive Transitions) yaani Simba walikuwa wakizuia na kumshinikiza mpinzani kukosea ili wapore mpira na kujibu shambulizi, ambapo Chama amefunga goli 3 kwa kushambulia nafasi baada ya Simba kupora mpira, mfano ni magoli dhidi ya Yanga SC, JKT Tanzania, Mashujaa na Tanzania Prison huku yeye mwenyewe akipika mawili dhidi ya Coastal Union na Tanzania Prisons.

 

 

 

Magoli matatu kati ya aliyoyafunga yamepikwa na Ellie Mpanzu ambaye amekuwa akisimama naye kwenye mstari wa mbele wa uzuiaji, wakipora mpira tu wote hushambulia nafasi kwa haraka, mmoja akiwa na mpira mwingine akishambulia nafasi.

 

 

 

 

 

Magoli matatu yaliyobaki ameyachangia wakati wa mipira ya kutenga (Set Pieces) ambayo yote ni ya kona, akitoa pasi za magoli mawili dhidi ya Tanzania Prison na Coastal Union na yeye kufunga kona ya moja kwa moja dhidi ya Mashujaa FC.

 

 

 

Tujivunie uwepo wao kwenye Ligi yetu

 

Ni ukweli usiofichika kuwa kwenye ligi 5 bora Afrika, ni ngumu kuona kwenye ligi moja wachezaji  wa timu tatu za juu wa nafasi inayofanana wenye mwendelezo bora kama walivyofanya Feisal Salum, Allan Okello na Clatous Chama kwenye mwezi Mei wa Ligi kuu ya NBC, hakika tunapaswa kujivunia uwepo wao kwenye ligi yetu, tufurahie zaidi burudani kutoka kwao, tusiishie kuwashindanisha tu.

 

 

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet