Messi aishtaki Argentina kutumia picha yake kupiga pesa
Sisti Herman
November 18, 2026
Share :

Lionel Messi ameripotiwa kutaka Shirikisho la Soka la Argentina (AFA) kuacha kutumia picha na taswira yake katika shughuli mbalimbali za kibiashara na matangazo.
Hatua hiyo inadaiwa kuchochewa na mvutano wa kibiashara kati ya Messi na uongozi wa AFA unaoongozwa na rais Claudio ‘Chiqui’ Tapia, pamoja na tuhuma za kiutawala na kifedha zinazoikabili taasisi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na vyombo vya habari vya Argentina, Messi kupitia mawakili wake ameandaa barua ya kisheria inayotaka AFA kusitisha matumizi ya jina, picha na video zake katika matangazo, udhamini na shughuli nyingine za kibiashara bila makubaliano yake.
Moja ya sababu za malalamiko hayo ni madai kwamba AFA iliruhusu kampuni ya bia ya Argentina inayodhamini shirikisho hilo kutumia picha ya Messi katika kampeni ya matangazo, licha ya mchezaji huyo kuwa na mkataba wa kibiashara na kampuni pinzani ya Marekani.
Hata hivyo, hadi sasa Messi na uongozi wa AFA hawajatoa tamko rasmi kuhusu taarifa hizo.





