"Messi ni rafiki yangu mkubwa" - Neymar
Eric Buyanza
June 25, 2026
Share :

Nyota wa soka wa Brazil, Neymar, amemmiminia sifa nahodha wa Argentina, Lionel Messi, akimtaja kuwa mmoja wa marafiki zake wa karibu ndani na nje ya uwanja wa soka.
Neymar alitoa kauli hiyo baada ya Brazil kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Scotland na kufuzu hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia la FIFA 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo, mshambuliaji huyo alisema urafiki wake na Messi umeendelea kuwa imara kwa miaka mingi, huku akisisitiza kuwa nyota huyo wa Argentina ana tabia njema hata nje ya uwanja.
“Ni mzuri uwanjani, hebu fikiria alivyo nje ya uwanja. Ni rafiki mkubwa sana. Anajua kwamba ninamjali sana,” alisema Neymar.
Kauli ya Neymar imeonyesha uhusiano wa karibu uliopo kati ya nyota hao wawili wa soka duniani, ambao waliwahi kucheza pamoja katika klabu ya FC Barcelona na baadaye kuungana tena katika klabu ya Paris Saint-Germain.
Licha ya kuwa wanatoka katika mataifa yenye ushindani mkubwa wa soka barani Amerika Kusini, Neymar na Messi wameendelea kudumisha urafiki wao na kuheshimiana ndani na nje ya mchezo huo.





