pmbet

"Mgao wa umeme wapungua kwa 80%, Machi utaisha" - Biteko

Sisti Herman

February 25, 2024
Share :

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa megawati  2,115  umeanza kazi na kuingiza  megawati 235 katika gridi ya Taifa kupitia mtambo Namba 9.

Hatua hii ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali kuwa mtambo huo ungeanza kuzalisha umeme tarehe 25 Februari 2024, ahadi iliyotimizwa siku tatu kabla kuanzia tarehe 22 Februari 2024  mtambo huo ulipoanza uzalishaji.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 25 Februari 2024 wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa baadhi ya wakuu wa vyombo vya Habari na Wahariri katika eneo la mradi wilayani Rufiji mkoani Pwani ambapo wahariri hao walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Bwawa la kuhifadhi maji yatakayozalisha umeme, Tuta Kuu na mitambo ya umeme.

Ameeleza kuwa, kuingia kwa megawati 235 kwenye Gridi ya Taifa  kumeboresha hali ya upatikanaji umeme nchini na kupunguza upungufu wa umeme kwa zaidi ya asilimia 85.

Ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere unaendelea na ifikapo mwezi  Machi 2024 megawati nyingine 235 zitaingia katika gridi kupitia mtambo namba 8 na kufanya JNHPP kuingiza megawati 470 kwenye gridi na hivyo kupelekea nchi kuwa na ziada ya umeme ya megawati 70.

Amesema utekelezaji wa mradi huo ni jitihada za Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye alikuta mradi huo ukiwa na aslimia 33 na sasa  mradi huo unafikia mwisho.

Amesema, Dkt. Samia anaijali nchi kwa dhati na sasa mipango yake ya maendeleo haiangalii kipindi cha sasa tu bali miaka 30 hadi 40 ijayo na ndio maana ameshaagiza uendelezaji wa vyanzo vipya vya umeme ikiwemo Gesi, Maji na Nishati Jadidifu inayojumuisha Jua, Upepo na Jotoardhi.

Dkt. Biteko pia amepongeza juhudi za Serikali ya  Awamu ya Tano chini ya Hayati, Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wa kutekeleza mradi huo ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2018.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameeleza kuwa, utekelezaji wa JNHPP hauifanyi Wizara ya Nishati na Taasisi zake kubweteka na kutegemea umeme kutoka mradi huo pekee bali kasi ya utekelezaji wa miradi mingine mipya inaendelea.

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet