Michael Carrick au Ole Gunnar Solskjaer kukabidhiwa Man U leo
Eric Buyanza
January 12, 2026
Share :
Imeripotiwa kwamba Manchester United wanatarajiwa kufanya uamuzi kuhusu meneja wao mpya wa muda leo Jumatatu Januari 12.
Mashetani hao wekundu waliondolewa kwenye raundi ya tatu ya Kombe la FA na Brighton Jumapili, na huenda huo ndio ulikuwa mchezo wa mwisho wa Darren Fletcher akiwa kocha.
Mashabiki wameachwa wamechanganyikiwa na matokeo hayo ikizingatiwa kuwa Ligi Kuu sasa ndiyo mashindano pekee ambayo timu hiyo imesalia nayo.
Fletcher aliteuliwa kama kocha wa mpito mara tu baada ya kufukuzwa kwa Ruben Amorim, ingawa United iliripotiwa kuwa ilikuwa ikifanya mazungumzo na makocha wengine.
Kwa mujibu wa talkSPORT, leo Jumatatu itakuwa siku muhimu ya kumpata meneja mpya wa mpito, huku Michael Carrick na Ole Gunnar Solskjaer wote wakiwa wamefanya mazungumzo na uongozi wa klabu kufukuzia kibarua hicho.






