Miili ya watu wanne yaokotwa kando ya barabara Kibaha.
Joyce Shedrack
October 16, 2025
Share :
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limethibitisha kutokea kwa vifo vya wanaume 4 ambao miili yao imekutwa pembezoni mwa barabara ya Mapinga kuelekea Kibaha, ikiwa na majeraha usoni na miguuni huku ikikadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 19 hadi 22, ambao walikuwa ni wakazi wa maeneo ya Dar es Salaam.
Kupitia taarifa iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani imeeleza kuwa Miili hiyo ilisafirishwa hadi Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa uchunguzi zaidi na baadaye, wazazi na ndugu waliweza kuitambua miili hiyo ya vijana wanne kuwa ni wakazi wa Dar es Salaam, ambao ni Mikidadi Abbas Mikidadi (21), Hassan Juma Jumanne (21), Fadhili Patrick Hiyola (19) na Abdalla Fadhil Nyanga (21).
Taarifa hiyo imebainisha kuwa miili hiyo imekabidhiwa kwa familia kwa taratibu za mazishi baada ya uchunguzi wa kitabibu kukamilika huku uchunguzi wa kina kubaini mazingira na wahusika wa mauaji hayo ukiendelea.
Jeshi la Polisi mkoani Pwani limetoa wito kwa wananchi kutoa taarifa yoyote inayoweza kusaidia kufichua ukweli wa tukio hilo na kusisitiza kuwa ushirikiano wa jamii ni muhimu ili kubaini kilichotokea na kuwachukulia hatua kwa waliosababisha vifo hivyo.