Misri yataka waliochezesha mechi yao na Argentina watimuliwe
Eric Buyanza
July 8, 2026
Share :

Shirikisho la Soka la Misri (EFA) limetangaza kuwa limewasilisha malalamiko rasmi kwa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), likitaka waamuzi waliosimamia mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia dhidi ya Argentina waondolewe kwenye mashindano hayo.
Malalamiko hayo yanahusiana na uamuzi wa teknolojia ya Video (VAR) uliobatilisha bao la Mostafa Zico wakati Misri ikiwa inaongoza kwa mabao 1-0 kipindi cha pili. VAR ilibaini kuwa kiungo Marwan Attia alimkanyaga Lisandro Martínez mwanzoni mwa shambulizi lililozaa bao hilo.
Aidha, Misri imeeleza kuwa nahodha wake Mohamed Salah alifanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari la Argentina, lakini mwamuzi hakutoa penalti.
Sekunde chache baadaye, Argentina ilianzisha shambulizi lililozaa bao la ushindi katika dakika za nyongeza.
Argentina iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Misri na kufuzu hatua inayofuata ya mashindano, huku EFA ikisisitiza kuwa maamuzi ya waamuzi yalikuwa na mchango mkubwa katika matokeo ya mchezo huo.





