Mjue mtoto mwenye nywele mwili mzima, mama ahofia laana
Eric Buyanza
April 11, 2024
Share :
Jaren Gamongan wa nchini Ufilipino ni mtoto aliyezaliwa tofauti kidogo na watoto wengine, kwani yeye alizaliwa akiwa na nywele mwili mzima na anatajwa kama mtoto mwenye nywele nyingi zaidi duniani huku mama yake akiamini alipata mimba yenye laana.
Mama yake aitwae Alma, anaamini alizaa mtoto huyo kama laana baada ya kula nyama ya 'paka wa porini' kipindi akiwa na mimba ya mwanae huyo.
Licha ya imani ya Alma lakini hakuna ushahidi wowote wa kisayansi unaothibitisha ulaji wa paka ungeweza kusababisha hali kama hiyo.
Alma anasema kipindi cha mimba ya Jaren alikuwa akijisikia hamu ya ajabu ya kula nyama ya 'paka pori' ambayo kwao Ufilipino ni nyama pendwa na hupatikana mbali kidogo milimani huko karibu na eneo analoishi.
Anaendelea kwa kusema majirani zake waliendelea kumjaza kwa story za kutisha kuhusu laana kutokana na kula nyama hiyo wakati wa ujauzito, lakini katika siku za karibuni alipompeleka mtoto huyo kwa daktari waligundua alikuwa na ugonjwa unaoitwa 'Hypertrichosis'.
Ugonjwa huo ni wa nadra sana na inakadiriwa humpata mtu mmoja katika kila watu "bilioni moja".
Alma ana wasiwasi mkubwa kuwa sura yake ya kipekee itakuwa changamoto shuleni.
"Nina wasiwasi naye sana wakati atakapokwenda shule, anaweza kunyanyapaliwa kwa kuwa tofauti na wenzake".
"Nilijilaumu sana alipozaliwa kwa sababu ya tamaa ya nyama ya paka niliyokuwa nayo. Nilijiona mkosaji sana.......Lakini hivi majuzi madaktari waliniambia kuwa nyama hiyo haihusiani na lolote."
"Nilikuwa nikijaribu kumpunguza hizo nywele, lakini nikagundua nikipunguza ndio zinaota nyingi zaidi.....tuliacha kumkata," anamalizia Alma.