Mjue mwanamke aliyefyatua risasi 8 na kuua mbele ya mahakama
Eric Buyanza
July 22, 2026
Share :

Mwaka 1981 mwanamke aliyefahamika kwa jina la Marianne Bachmeier wa nchini Ujerumani alipata umaarufu mkubwa duniani baada ya kumuua kwa risasi ndani ya mahakama mtuhumiwa Klaus Grabowski, mwanaume aliyekuwa anatuhumiwa kwa kumbaka na kumuua binti yake wa miaka saba, Anna Bachmeier.
Kisa hiki kinachukuliwa kuwa moja ya matukio maarufu zaidi ya kulipa kisasi (vigilante justice) katika historia ya sheria nchini Ujerumani.
ILIKUWA HIVI;
Mnamo tarehe 5 Mei 1980, mtoto wa Marianne aitwaye Anna alitofautiana na mama yake na kuamua kutokwenda shule, lakini baadae alitekwa na mfanyakazi wa bucha aitwae Klaus Grabowski ambaye alimbaka na kisha kumnyonga kwa kutumia soksi kabla ya kuufungia mwili wake kwenye sanduku na kulitupa kando ya mfereji wa barabara. Hata hivyo baadae alikamatwa na polisi na kukiri kosa la mauaji.
Siku ya tatu ya kesi hiyo, mama wa binti alifanikiwa kuingia mahakamani kinyemela akiwa na bastola aliyokuwa ameificha kwenye koti alilovaa.
Wakati kesi inaendelea huku Grabowski akiwa amekaa kwenye benchi la mahakama, Marianne alisimama ghafla akatoa bastola na kumfyatulia Grabowski risasi 8 za mgongo na kufariki papo hapo.
Baada ya kufanya tukio hilo, Marianne alinukuliwa akisema: "Nimemuua kwasababu alimuua binti yangu."
Kitendo hicho kilizua mjadala mkubwa sana nchini Ujerumani na kote duniani. Sehemu kubwa ya jamii ilimuona Marianne kama shujaa aliyechukua hatua baada ya kuona mfumo unalegalega (kwani Grabowski alikuwa ameachiliwa huru huko nyuma licha ya makosa ya awali ya unyanyasaji wa watoto). Wengine walimlaumu kwa kuvunja sheria na kuzuia haki isitendeke mahakamani.
Machi 1983, mahakama ilimkuta Marianne na hatia ya mauaji ya bila kukusudia na umiliki wa silaha kinyume cha sheria. Alihukumiwa kifungo cha miaka sita jela. Hata hivyo, alitumikia kifungo hicho kwa miaka mitatu tu kabla ya kuachiliwa huru kwa dhamana mnamo Juni 1985.





