Mke anaswa akidandia lori ili kumfumania mumewe
Eric Buyanza
April 18, 2026
Share :

Katika hali ya kushangaza mwanamke mmoja huko nchini China aliyefahamika kwa jina la Bi. Yu ambaye alikuwa akimshuku mumewe kuwa huenda akawa sio mwaminifu na labda ana mwanamke mwingine alinaswa na kamera akitumia njia za kimafia ili kumfumania mwanaume huyo.
Video na picha zilizopigwa na madereva barabarani zilionyesha mwanamke huyo akishikilia vyuma nyuma ya lori lililokuwa likitembea, lakini sababu zake hazikujulikana hadi polisi wa eneo hilo walipotoa taarifa kuwa yote hayo yalisababishwa na wivu wa kimapenzi.
Polisi waliposimamisha lori hilo walibaini kwamba mwanamke aliyekuwa akining’inia nyuma ya lori alikuwa mke wa dereva ambaye aliamua kumnyatia mumewe wakati akitoka nyumbani usiku ili kumfuatilia.
Polisi wanasema ilikuwa ni bahati kubwa kwa mwanamke huyo kuwa hai kwani mume wake alikuwa akiendesha lori hilo kwa mwendo wa kasi sana.
Bi. Yu, aliishia kumtia hasara mumewe ambaye alipigwa faini na polisi kwa kushindwa kukagua vizuri lori lake kabla ya kuondoka nyumbani.





