Mkuu wa Jeshi la Polisi Kenya akubali kuachia ngazi.
Joyce Shedrack
July 12, 2024
Share :
Inspekta Jenerali wa polisi nchini Kenya Japhet Koome amejiuzulu nafasi yake ya kuliongoza Jeshi hilo kufuatia wiki kadhaa za maandamano yenye ghasia ambapo zaidi ya watu 40 waliuawa.
Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed amesema kupitia taarifa kwa vyombo vya habari kwamba Koome aliwasilisha barua ya kujiuzulu kwa Rais William Ruto na Rais ameridhia ombi lake.
“Mheshimiwa William Samoei Ruto, Ph.D, CGH, Rais na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, mnamo Julai 12 2024, amekubali kujiuzulu kwa Mhandisi Japheth N Koome, MGH, kama Inspekta Jenerali wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi,” ilisema taarifa hiyo.
Rais Ruto amemteua Douglas Kanja kuwa kaimu Inspekta-Jenerali wa Huduma ya Polisi ya Kitaifa hapo awali Kanja alikuwa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi.
Bw Eliud Langat atakuwa Kaimu Naibu Inspekta Jenerali, Huduma ya Polisi ya Kenya huku Bw James Kamau akiwa Kaimu Naibu Inspekta Jenerali, Huduma ya Polisi wa utawala.
Baada ya maandamo yaliyotokea Nchini humo kumekuwa na shinikizo kubwa la kutaka Koome ajiuzulu kutoka kwa vijana ambao wamekuwa wakiandamana maarufu kama Genz hasa baada ya kubainika baadhi ya watu kuuawa kwa risasi na mabomu ya machozi wakati wa maandamano.