Mnyama kuzindua jezi mpya za msimu Agosti 27.
Joyce Shedrack
August 20, 2025
Share :
Klabu ya Simba imetangaza rasmi itafanya uzinduzi wa jezi mpya za Msimu tarehe 27/8/2025 katika Ukumbi wa Super Dome Masaki Jijini Dar es Salaam.
Kiingilio cha kushiriki tukio hilo kwa mtu yeyote atakayehitaji ni Sh.250,000 laki mbili na nusu kwa mtu mmoja na atakayeshiriki kwenye uzinduzi huo atapata jezi zote tatu za msimu pamoja na vitu vingine vitakavyopatikana siku hiyo ndani ya ukumbi wa Super Dome.
“Jezi za Simba msimu huu tutazindua kwa namna tofauti kidogo, ipo namna ambayo tumezoea jezi huwa zinazinduliwa lakini safari hii sababu tuna mdhamini mpya wa jezi kampuni ya JayRutty akishirikiana na kampuni ya kimataifa ya Diadora tukaamua kufanya kitu kipya chenye mvuto kwa jamii na biashara ya jezi kuwa na mvuto wa tofauti.”
“Jezi za Simba SC msimu wa 2025/26 zitazinduliwa tarehe 27/Agosti/2025, jezi zitazinduliwa majira ya saa 1:00 usiku na shughuli itafanyika kwenye ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki. Safari hii tumefanya kuwa tukio lenye kubwa, tukio lenye hadhi ya ushua na kulifanya kuwa tukio bora ambalo litakutanisha wadau wakubwa wa Simba Sports Club na ambao wanataka kununua jezi ya Simba baada ya kuzinduliwa.” Ahmed Ally akizungumza na waandishi wa habari siku ya leo.