Moalin aeleza namna 'Midfield Variations' yake ilivyomtegemea Kenny
Sisti Herman
October 31, 2024
Share :
Baada timu yake kupata ushindi wa 1-0 nyumbani dhidi ya klabu ya Namungo kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara, kocha mkuu wa klabu ya KMC amemeelezea kiufundi ni kwa namna gani viungo wake wawili waliwapa ubora huku akimpongeza kiungo wake wa kati ambaye pia ni nahodha wa klbu hiyo Kenny Ally Mwambungu baada ya kuonyesha kiwango bora sana kwenye mchezo huo kiasi cha kubeba tuzo ya mchezaji bora wa mchezo inayotolewa na mdhamini mkuu wa ligi kuu Tanzania bara, benki ya NBC.
“Ni kweli mara nyingi huwa nawatumia Fred Tangalo na Paschal Mussa kama viungo wa kati na Kenny mbele yao (double Pivot), lakini leo nilianza na Kenny na Paschal ili nyakati tukiwa na mpira, wote wawili washiriki ujenzi wa shambulizi kuanzia nyuma (Kwenye umbo la Double Pivot) kisha tukiwa kwenye nusu ya wapinzani awe anasogea zaidi mbele usawa wa Redemtus na kumuacha Paschal mbele ya mabeki (wakiwa kwenye umbo la Single Pivot) kwasababu kiufundi Kenny mzuri zaidi kusaidia timu kupenya kuta za uzuiaji za wapinzani wetu na kutengeneza nafasi” Moalin alimwelezea mwandishi wa makala hii.
“Sababu za kucheza hivyo ni kwasasabu nilitaka kuona ni kwa namna gani watacheza na sisi kwenye miundo yote miwili, wakiwa wawili na akiwa mmoja chini na ilitusaidia kwasababu nyakati nyingi tuliwachanganya na hata viungo wao mara nyingi walibaki chini pindi Kenny anaposogea usawa Redemtus” aliongeza Moalin.
“Nyakati za kuzuia Kenny anarejea usawa wa Paschal na kucheza wawili mbele ya mabeki na waliwalinda vizuri” akapigilia msumari kuhusu kiwango cha Kenny.
Baada ya mchezo huo, KMC imepanda hadi nafasi ya 6 kwenye msimamo wa ligi baada ya kukusanya alama 14 kwenye michezo 10 iliyocheza huku wakiwa alama 10 nyuma ya vinara klabu ya Yanga.