pmbet

MOI yaanza upasuaji rekebishi wa viungo vilivyopooza

Eric Buyanza

February 12, 2026
Share :

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeanza kutoa huduma za upasuaji wa kibingwa wa kutibu mishipa ya fahamu iliyoathirika kwa ajali katika mikono na miguu (hand injury and soft tissue reconstruction) kwa wagonjwa wanaokabiliwa na changamoto hiyo.
 

Akizungumza leo Februari 10, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema hatua hiyo ni mafanikio makubwa kwa taasisi hiyo na sekta ya afya nchini kwa ujumla.
 

“Tumeanza kwa mafanikio kutibu mishipa ya fahamu iliyopo mikononi na miguuni. Huduma hii itawanufaisha wagonjwa wanaoshindwa kuinua vitu au wanaopata changamoto ya kutembea vizuri baada ya kupata ajali,” amesema Dkt. Mpoki.
 

Ameongeza kuwa upasuaji huo kwa sasa unapatikana katika taasisi ya MOI pekee kwa hapa nchini, baada ya madaktari wa taasisi hiyo kupata mafunzo ya ubobezi na ujuzi maalum wa kufanya upasuaji huo.
 

“Huduma hii imeanza baada ya daktari wetu kukamilisha masomo ya ubobezi na kupata utaalamu wa kutibu na kufanya upasuaji wa mishipa ya fahamu iliyopata majeraha,” ameongeza.
 

Kwa upande wake, Daktari Bingwa Bobezi wa Majeraha ya Mkono na Mguu, Dkt. Hellen Machagge, ameeleza kuwa tatizo la mishipa mikubwa ya fahamu kujeruhiwa husababisha misuli midogo kushindwa kufanya kazi, hali inayosababisha kupooza kwa mikono au miguu.

 

“Katika upasuaji huu tunahamisha mishipa ya fahamu kutoa sehemu moja kwenye sehemu iliyoathirika na kuuwezesha mkono au mguu kuanza kufanya kazi vizuri kama ilivyokuwa awali kabla ya kujeruhiwa” amesema Dkt. Hellen
 

Huu ni muendelezo wa Taasisi ya MOI kuendelea kuanzisha huduma za kibingwa na kibobezi ambazo hazipatikani hapa nchini na kuwaondolea usumbufu na gharama kubwa ya fuata huduma hiyo nje ya nchi.


 

Na Erick Dilli- MOI

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet