Moto wateketeza soko la Temeke Stereo
Eric Buyanza
June 14, 2025
Share :
Soko maarufu la Temeke Stereo jijini Dar es Salaam limeteketea kwa moto mkubwa usiku wa kuamkia leo, na kusababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara waliokuwa wakitegemea eneo hilo kwa shughuli zao za kila siku.
Moto huo ulioanza majira ya usiku umeharibu mabanda, bidhaa, na mali mbalimbali, huku juhudi za kuuzima zikihusisha Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama. Chanzo cha moto bado hakijafahamika rasmi, ingawa mashuhuda wamedai huenda kilihusisha hitilafu ya umeme au uzembe wa kibinadamu.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, baadhi ya wafanyabiashara wamesema wamepoteza kila kitu, na wameiomba Serikali iwasaidie kurejea katika hali yao ya kawaida ili waweze kuendeleza shughuli za kujitafutia kipato.
Vikosi vya zimamoto vilifika eneo la tukio na kufanikiwa kudhibiti moto kabla haujasambaa zaidi, ingawa mlundikano wa mabanda na miundombinu duni vilikwamisha juhudi za awali.
Mamlaka za wilaya ya Temeke zimeahidi kufanya tathmini ya hasara na kuanza mchakato wa kuwasaidia waathirika wa tukio hilo.
HabariLeo