pmbet

Mrembo kinda wa Tanzania anayekichafua Basketball Uganda

Sisti Herman

December 26, 2023
Share :

Wakati wahenga wa kiswahili wanakuja na msemo maarufu wa “mshika mawili, moja humponyoka” kauli yao haikukataza mtu kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja bali ilikuwa ikikumbusha nidhamu wakati wa kufanya mambo hayo kwa wakati mmoja ili yafanywe kwa ufasaha, kwani bila nidhamu kuna uwezekano wa kufeli kufanya moja au yote kwa pamoja.

 

Wachezaji wengi ambao wamejaribu kufanya michezo na vitu vingine kwa wakati mmoja kama biashara, masomo au kazi wameishia kushindwa kwenda navyo kwa mwendo sawa na imeshuhudiwa wengi wakiacha mmoja kati ya hayo na kubaki na lingine, yaani kama ni michezo ni michezo tu, kama ni masomo ni masomo tu au kama ni biashara ni biashara tu.

 

PM Sports imekuandalia makala fupi ya mahojiano maalum na binti mrembo ambaye kwa kimo chake huwezu kuamini kama anatajwa kuwa lulu ya taifa kwenye mchezo wa mpira wa kikapu siku za usoni aliyejitoa kwa nidhamu kubwa kushika mambo mawili ambayo yamewashinda wengi, Michezo na Elimu ambaye amecheza michuano mikubwa ya mpira wa kikapu ingali akiwa na umri mdogo Naima Omary

 

Umuhimu wachezaji kuwa na elimu?

 

“Ni muhimu kwa mchezaji kuwa na elimu kwasababu ukiwa na elimu ni rahisi kuelewa mambo mengi ya kimichezo kama kuelewa haraka mbinu za makocha, lugha za kufundishia na kuwasiliana na makocha au wachezaji wa nchi tofauti, namna ya kuwasiliana, kuelewa sheria za mchezo na hata masuala ya afya na milo, ni muhimu sana kwa mwanamichezo, hapo unaweza kuwa mweledi” alianza kupangua maswali ya mwandishi wa PM Sports, Naima ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha 6 kwenye shule ya sekondari St. Mary Kitende ya nchini Uganda ambayo pia humiliki klabu ya Vipers ya ligi kuu nchini humo.

 

Ni ngumu kuchanganya Elimu na masomo kwa wakati mmoja?

 

“Hapana, inategemeana na mgawanyo wa ratiba, nashukuru Mungu wazazi wangu waliliona hilo mapema na kuchagua nisome shule ambayo ina mgawanyo mzuri wa muda wa kusoma na kucheza ili nipate elimu kwenye daraja ninalo stahili wakati huohuo nijiendeleze kimichezo na hapo jukumu langu linakuwa kuishi kwenye nidhamu sahihi ya kufuata muda kulingana na ratiba za masomo na shule” alijibu Naima ambaye  pia ni Mchezaji bora wa kike (MVP) wa mradi wa kuibua vipaji vya mchezo wa mpira wa kikapu na kuviendeleza uitwao SEED PROJECT TANZANIA.

 

Basketball haiathiri ratiba zako kitaaluma?

 

“Haiathiri, sanasana inaniongezea juhudi na uwezo wa kufikiria zaidi, athari huja pale unaposhindwa kuwa na nidhamu na ratiba na hapo nio utakuata muda wa masomo unajikuta umechoka kwasababu ya mazoezi lakini kama ukiwa na nidhamu nzuri ya muda wa mazoezi, kupumzika na kusoma haina athari yoyote, nidhamu tu” alisisitiza Naima ambaye pia huchezea timu ya Basketball ya Mchenga Queens ya Dar es salaam inayofundishwa na kocha Muhhamed Yusuph pia hushiriki michuano ya kitaifa ya Basketball nchini.

 

Ukiwa Tanzania unashiriki mashindano na timu yako?

 

“Ndiyo, nimeshiriki mashindano ya kikapu ya RBA (mashindano ya Basketball ya mkoa wa Dar es salaam, Tanzania) na Taifa Cup lakini pia nilishawahi kuchaguliwa kushiriki ZONE 5 (Mashindano ya Basketballl yanayoshirikisha timu kutoka mataifa mbalimbali) lakini nkashindwa kucheza kwasababu nilikua na umri mdogo, walihitaji wasichana kuanzia miaka 18 na zaidi” alisema kwa kusikitika kinda Naima ambaye ni mzaliwa wa Julai 20 mwaka 2005.

 

Kuna utofauti wa mashindano ya shule Uganda na Tanzania?

 

“Upo, huku shule nyingi zinafanana uendeshaji na ratiba rafiki kwa mchezaji, pia zina mashandano mengi hivyo mfanano wa ratiba na kuwa kwenye mashindano mara kwa mara huweka mazingira ya kuwa timamu mara zote kushindana na kumjenga mchezaji ndiyo maana mashindano mengi ya FEASSA mabingwa huwa timu za Uganda (mashindano ya mashirikisho ya shule Afrika mashariki)” aliendelea Naima ambaye anasoma tahasusi ya masomo ya biashara kama Ecomomics, Geography na Mathemetics.

 

Kimo chako siyo kikwazo kwa Basketball?

 

“Hapana, mimi naona ndiyo nakuwa mchezaji mzuri kwa kimo changu” alijibu kinda huyo mwenye urefu wa futi 5 na inchi 4 sawa na sentimita 164, kimo ambacho kwa aina ya wachezaji wa Basketball wengi ni kufupi lakini yeye ameonekana kuwa huru zaidi hata aina ya magoli ambayo amekuwa akifunga ni yale ya mbali ambayo hayategemei kimo zaidi ya ufundi na kukadiria vipimo na nguvu za mikono.

 

Wasichana hupitia vishawishi vya kimapenzi michezoni kwako vipi, unakwepaje?

 

“Kiukweli, vishawishi vipo ila havijawahi kuniathiri kutokana na misimamo na mipaka yangu niliyojiwekea na kila mtu kuanzia wachezaji wenzangu wa kike na wa kiume, makocha na waalimu au hata marafiki ambayo siyo rahisi mtu kuvuka mpaka wa mahusiano na akivuka ina maana amenivunjia heshima” alihitimisha na jibu hili Naima ambaye hucheza kama Point Guard awapo uwanjani, nafasi ambayo huchezwa na wachezaji wenye vimo vifupi na wenye uwezo mkubwa kukaa na mpira na kupiga pasi kwa wenzao, mara nyingi huwa wachezaji wa timu kiufundi.

 

 

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet