Msumbiji kusaka ushindi wake wa kwanza AFCON 2025.
Joyce Shedrack
December 24, 2025
Share :
Msumbiji inaamini inaweza kupambana na kutinga hatua ya mtoano katika Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) la 2025, hii ni kulingana na mchezaji wa zamani wa Kimataifa Manuel Bucuane.

Msumbiji wanaojulikana kama The Mambas hawajawahi kusonga mbele katika hatua ya makundi katika mashindano matano yaliyopita na bado wanasubiri ushindi wao wa kwanza katika fainali, wakiwa wametoka sare tano na kupoteza mechi 10 kati ya 15 zilizopita.
Kikosi cha kocha Chiquinho Conde kinakabiliwa na jukumu gumu katika Kundi F dhidi ya mabingwa watetezi Ivory Coast, mabingwa mara tano Cameroon na timu ya Gabon inayoongozwa na Pierre-Emerick Aubameyang, lakini Bucuane anabaki na matumaini.
"Msumbiji haichezi katika hatua hizi kila wakati kwa hivyo kila wakati timu inapofuzu, ni mafanikio makubwa kwa nchi," mshambuliaji huyo mstaafu aliambia BBC Sport Africa.
"Timu inakua, kuna vijana wengi wanaochipukia.Tuna wachezaji wanaoonyesha kwamba wanaweza kushindana katika kiwango cha juu zaidi."
"Tunatumai kwamba kwa mara ya kwanza tunaweza kushinda mechi au hata kusonga mbele hadi hatua inayofuata.
"Haitakuwa rahisi. Tuko katika kundi gumu sana lenye nchi zenye nguvu sana, lakini tunawaamini vijana hawa."
Mambas wataanza kampeni yao dhidi ya Ivory Coast Jumatano hii saa mbili na nusu usiku kwa saa za Afrika Mashariki kabla ya mechi dhidi ya Gabon (28 Desemba) na Cameroon (31 Desemba).





