Mswati amposa binti wa Zuma mwenye miaka 21
Sisti Herman
July 15, 2024
Share :
Mfalme Mswati wa taifa la Swaziland "Eswatini" anadaiwa kuwasilisha posa ya kimila ya Ng'ombe 10 "Kucela" kwa familia ya aliyewahi kuwa Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma kwaajili ya kumuoa binti wa Rais huyo Nomcebo Zuma mwenye umri wa miaka 21
"Kucela" ni neno la kiSwati na katika muktadha, linamaanisha kuomba ruhusa kutoka kwa wazee, wazazi au walezi kabla ya kuoa binti yao.
Uchunguzi uliofanywa na shirika la Habari la Swaziland uligundua rekodi za uhamiaji zinazoonyesha, Nomcebo Zuma alikuwa akitembelea eSwatini mara kwa mara kuanzia tarehe 13 Machi 2024 kupitia mpaka wa Lavumisa na Oshoek-Ngwenya.
Rekodi zinaonyesha zaidi kwamba Nomcebo Zuma sasa anatumia muda wake mwingi katika Ufalme wa eSwatini.
Lakini takriban mwezi mmoja uliopita, rekodi za uhamiaji zinaonyesha kwamba, anayedaiwa kuwa 'Liphovela' aliwasili nchini na wiki chache baadaye, Mfalme anadaiwa kuwatuma watu wake wa jadi kuomba ruhusa kutoka kwa familia ya Zuma huko KwaZulu-Natal ili aweze kumuoa anayedaiwa kuwa Liphovela. .
Katika lugha ya eSwatini "Liphovela" ni mchumba rasmi wa Mfalme ambaye yuko karibu kuolewa na kujiunga na familia ya kifalme.
Jina la Nyumba ya Wageni ambako anayedaiwa kuwa Mfalme Liphovela amewekwa linajulikana kwa mwandishi wa habari hii lakini haliwezi kutajwa kwa sababu za kiusalama.
Alipohojiwa na gazeti la Swaziland News Msemaji wa Mfalme Percy Simelane alisema hakuwa na habari kuhusu mapendekezo ya ndoa kati ya Mfalme Mswati na binti wa Zuma.
Kama ilivyoripotiwa na gazeti hilo, inadaiwa kuwa, takriban wiki mbili(2) zilizopita, Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma alipuuza mkutano wa familia ulioandaliwa kwa ajili ya mila ya "kucela".
Kiongozi huyo wa zamani wa Taifa la Afrika Kusini anadaiwa kukataa kuhudhuria mkutano wa familia, kwa vile alihisi kusalitiwa na ‘rafiki’ wake.
Mswati, Mfalme mwenye ndoa ya wake wengi zaidi ya kumi na tano(15), anadaiwa kwanza kumwambia Jacob Zuma kwamba, binti huyo ataolewa na mmoja wa wanawe wa kiume.