Muhoozi amps dhamana Besigye
Sisti Herman
October 31, 2026
Share :

Juhudi za kutafuta suluhu kuhusu hatima ya mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Uganda, Dk Kizza Besigye, zimechukua mwelekeo mpya baada ya Jenerali Salim Saleh kufichua kuwa ameanza kushughulikia suala hilo kufuatia ombi la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Muhoozi Kainerugaba, huku akitarajia matokeo ndani ya miezi mitatu hadi sita ijayo.
Saleh, ambaye ni mshauri mkuu wa Rais katika masuala maalumu na Mratibu Mkuu wa Operesheni ya Utajirisho (Operation Wealth Creation), amesema amerejea kuwasiliana na Besigye baada ya miaka kadhaa ya kutokuwa na uhusiano wa karibu kutokana na tofauti zao za kisiasa.
Akizungumza Oktoba 30, 2026, mbele ya viongozi wa kamati za Bunge, wabunge na viongozi wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM), katika kituo chake cha Kapeeka, Wilaya ya Nakaseke, Saleh alisema hatua yake ilianza baada ya kuona ujumbe uliowekwa na Muhoozi kwenye mtandao wa kijamii wa X, Agosti 25, 2026.
Alisema katika ujumbe huo, Muhoozi alielekeza kuwa suala la Besigye lishughulikiwe na Saleh, jambo lililomfanya awasiliane naye ili kuthibitisha kama alikuwa na nia ya kweli.
“Niliuona ujumbe huo Agosti 25 kutoka kwa kiongozi wa Patriotic League of Uganda (PLU), Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
“Alisema tatizo la Kizza Besigye ni langu. Kwangu mimi, hakujua kuwa alikuwa amenipa fursa nzuri sana ya kuungana tena na rafiki yangu wa zamani,” alisema Saleh.





