Mume atumia 'Droni' kumnasa mkewe aliyekuwa akichepuka
Eric Buyanza
July 24, 2024
Share :
Mwanamume mmoja huko China alimnasa mkewe aliyekuwa akichepuka na bosi wake wakati wa kazi, kwa kutumia ndege isiyo na rubani (Drone) kwa ajili ya kuwapeleleza wawili hao.
Mwanaume huyo aliyefahamika kwa jina la Jing alianza kumshuku mke wake kuwa ana uhusiano wa kimapenzi nje baada ya mwanamke huyo kuanza kubadilika kitabia jambo lililomfanya Bwana Jing kuanza upelelezi.
Jing aliamua kutumia ndege isiyo na rubani kumpeleleza mke wake kwa umakini mkubwa huku akihakikisha hakuna atakayemgundua anachokifanya.
Siku moja, alipokuwa kwenye upelelezi wake alimwona mke wake akitoka ofisini na mtu asiyeeleweka na kuingia naye kwenye gari.
Waliondoka kwa gari hadi eneo la mbali la milimani ambapo ndege isiyo na rubani iliwakamata wakiwa wameshikana mikono na kuelekea kwenye nyumba mbovu mbovu iliyojificha. Dakika 20 baadaye, wawili hao walitoka nje ya nyumba na kurudi mahali pao pa kazi.
Jing baadaye aliingia kwenye mitandao ya kijamii na kuripoti kwamba mwanamume aliyenaswa kwenye video na ndege yake isiyo na rubani alikuwa bosi wa mkewe, na kuchapisha picha zao wakiwa wameshikana mikono na kusema angetumia picha hizo za 'Drone' kama ushahidi wa kupata talaka.