Mvua kubwa yaja Dar, Pwani, Kusini na Morogoro
Eric Buyanza
May 2, 2024
Share :
Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini imetoa tahadhari ya uwepo wa mvua kubwa katika mikoa Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro, Dar es Salaam na maeneo ya jirani itakayosababishwa na mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Hindi Mashariki mwa Pwani ya Mtwara.
Taarifa hiyo ya mgandomizo huo mdogo wa hewa ambayo imetolewa na mamlaka hiyo imeeleza kuwa mgandamizo huo unatarajiwa kuimarika na kufikia hadhi ya Kimbunga kamili hadi kufikia Mei 2, 2024 na wakati mgandamizo huo mdogo wa hewa ukiendelea kuimarika, unatarajiwa pia kusogea kuelekea baadhi ya maeneo ya Pwani ya nchi yetu kuanzia usiku wa kuamkia siku ya Ijumaa Mei 3, 2024.
Mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kuendelea kuwepo katika maeneo ya Ukanda wa Pwani ya nchi yetu hadi Mei 6, 2024.
Hata hivyo, mgandamizo huo mdogo wa hewa unatarajiwa kupungua nguvu baada ya Mei 6, 2024.
Wananchi wameshauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa mgandamizo huo mdogo wa hewa na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa mara kwa mara kila inapobidi.