Mwakinyo kupasuana na Mzimbabwe visiwani Zanzibar
Eric Buyanza
January 2, 2024
Share :
Bondia Hassan Mwakinyo Januari 27 mwaka huu anatarajiwa kupanda ulingoni kuzichapa na bondia kutoka Zimbabwe Enock Msambudzi kwenye pambano lililopewa jina la ‘Mtata Mtatuzi’ huko visiwani Zanzibar.
Pambano hilo litapigwa kwa mara ya kwanza katika uwanja mpya wa ndani wa masumbwi ‘indoor arena’ ndani ya Uwanja mpya wa Amaan complex.
Kwa upande wake, Mwakinyo amesema yupo katika maandalizi mazuri kuelekea pamabano hilo ambalo mipango inaendelea kuhakikisha linakuwa na mkanda wa Shirika la Masumbwi Ulimwenguni (WBO).
“Nipo katika maandalizi mazuri sana. Nimejihakikishia hakuna atakayejuta kunishabikia,” amesema Mwakinyo
Naye, balozi wa pambano hilo, James Tupatupa amesema pambano la Mwakinyo limebeba taswira ya mapinduzi kutokana na uimara na umahiri wa bondia huyo.
“Mapinduzi rasmi ya ngumi yanaenda kufanyika Zanzibar, kwani linaenda kuwa zaidi ya pambano la kawaida,” amejinadi Tupatupa
Jumla ya mapambano 11 yanatarajiwa kushuhudiwa siku hiyo ambapo wanamasumbwi kutoka mikoa ya Zanzibar, Mbeya, Tanga na Dar es Salaam wanatarajiwa kuburudisha usiku huo.