Mwamuzi aanguka uwanjani kisa joto kali Copa Amerika
Sisti Herman
June 26, 2024
Share :
Wakati mechi kati ya Peru dhidi ya Canada ikiendelea kwenye michuano ya kombe la mataifa Amerika (Copa-America) mwamuzi msaidizi Humberto Panjoj aliyekuwa alianguka uwanjani kutokana na kuzidiwa na joto kali.
Mwamuzi huyo alidondoka dakika za mwisho za kipindi cha kwanza katika mchezo huo uliopigwa jana kwenye dimba la Children's Mercy Park.
Kwa mujibu wa tovuti ya The Sun News imeeleza kuwa baada ya kudondoka alitolewa na kupatia huduma ya kwanza na mpaka sasa bado haijafahamika hali yake inavyoendelea.
Hata hivyo inadaiwa kuwa Joto limekuwa kali sana nchini humo na kwa siku ya jana katika uwanja huo vipimo vilisoma ni nyuzi joto 38.
Wachezaji wa Canada wameonesha wasi wasi wa usalama wao kutokana na hali ya joto kwa sababu wamekuwa wakicheza mechi muda ambao jua bado linawaka.
Mmoja ya wachezaji ambaye ni beki, Alistair Johnston amesema ni mazingira ambayo hawatamani hata kukutana na wapinzani wao, hivyo ametaka wabadilishiwe muda wakuingia uwanjani.