Mwanafunzi adaiwa kuishi shule na ujauzito hadi kujifungua
Eric Buyanza
June 12, 2025
Share :

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, ametembelea Shule ya Wasichana Tabora kwa lengo la kuzungumza na uongozi wa shule hiyo pamoja na wazazi, kufuatia mfululizo wa matukio yaliyoibua sintofahamu kuhusu mwenendo wa nidhamu na uongozi katika shule hiyo ya kihistoria.
Akitoa taarifa rasmi ya uchunguzi, Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt. John Mboya, alieleza kuwa mwanafunzi wa shule hiyo ambaye jina lake na taarifa zake zimehifadhiwa kwa mujibu wa sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, alitoa taarifa ya kuumwa na akapelekwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa Kitete,lakini baada ya kupokelewa, kabla majibu ya vipimo vyake kutoka alibainika kuwa alijifungua katika maliwato ya hospitalini hapo hali ambayo iliulazimu uongozi wa wilaya na mkoa ukiongozwa na Katibu Tawala mkoa kuunda timu maalum kufanya uchunguzi juu ya hali hiyo na mwenendo mzima wa uendeshaji wa shule hiyo.
Taarifa ya uchunguzi ilibaini kuwa mwanafunzi huyo aliripoti shuleni hapo akiwa na ujauzito—lakini cha kushtua zaidi ni kuwa hakuna mwalimu wala kiongozi yeyote wa shule aliyeweza kugundua hali hiyo hadi kufikia hatua ya kujifungua.
“Tabia ya baadhi ya wanafunzi kujihusisha na ngono wakiwa bado shuleni ni jambo linaloumiza sana. Wazazi tunapaswa kushirikiana kwa nguvu katika malezi ya watoto wetu wa kike.”Alieleza Dkt. Mboya





