Mwanajeshi apigana vita wiki nzima akiwa na risasi iliyokwama kichwani
Eric Buyanza
March 15, 2025
Share :
Mwanajeshi mmoja wa kirusi amekuwa akitajwa kama shujaa wa nchi hiyo baada ya kupigana vita kwa wiki nzima hata baada ya kupigwa risasi ya kichwa na majeshi ya Ukraine wakati akipambania kuurejesha mji Kursk uliotekwa na vikosi vya Ukraine toka Agosti mwaka jana.
Mwanajeshi huyo ambaye jina lake halikutajwa, wa Kikosi cha 155 cha Wanamaji cha jeshi la Urusi, anasema akiwa kwenye mapambano aliona kofia yake ikirushwa juu kutoka kwenye kichwa chake, ambapo kwa hesabu zake za haraka alijiona mwenye bahati kuwa amekoswa na risasi iliyopiga kofia yake...asijue kuwa risasi hiyo ilimpata.
Anasema baada ya tukio hilo alianza kusikia maumivu pembeni ya jicho lake la kulia ambalo baadae lilivimba lakini aliendelea na mapambano akiamini uvimbe huo ungepona wenyewe.
Hata hivyo akiwa kwenye uwanja wa mapambano alipata jeraha lingine kubwa kutokana na makombora ya Ukraine na kulazimika kukimbizwa hospitali ambapo madaktari wa jeshi baada ya kumfanyia kipimo cha X-Ray waligundua risasi kubwa iliyokuwa imekwama kwenye ubongo wa askari huyo.
Kwa mujibu wa madaktari hao kilichotokea kwa askari huyo ni muujiza.