Mwanamke mbaroni kwa kukata nyeti za mpenzi wake
Eric Buyanza
July 25, 2024
Share :
Polisi katika Wilaya ya Kyotera nchini Uganda wanamshikilia mwanamke aliyefahamika kwa jina Harriet Ampayire mwenye umri wa miaka 23 akituhumiwa kukata uume wa mpenzi wake aitwaye Reagan Karamagi, kitendo kilichosababisha damu nyingi kumtoka hali iliyopelekea kifo chake.
Gazeti la Daily Monitor la nchini Uganda limeripoti kuwa, Harriet ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya kamari ya Fort Bet, katika mji wa Mutukula alitoroka baada ya kufanya ukatili huo usiku wa Jumapili tarehe 21.
Twaha Kasirye, Msemaji wa Polisi alithibitisha kukamatwa kwa Harriet Ampayire na kueleza kuwa atakabiliwa na mashtaka ya mauaji mara upelelezi utakapokamilika.
"Kwa kuwa tuna mpaka wa Mutukula, wahalifu huvuka kwa urahisi kila upande wa mpaka na mshukiwa alitumia fursa hiyo kuingia Tanzania. Hata hivyo tuna bahati kwamba tulifanikiwa kumkamata siku ya Jumanne," alisema msemaji huyo wa Polisi.
Bwana Valentino Yiga, ambaye alikuwa jirani wa marehemu akiongea kwa uchungu alisema;
"Ni upuuzi tumempoteza Reagan, alikuwa hawezi kupita bila kutusalimia. Mwanamke huyo tunamjua amekuwa akimtembelea mara kwa mara na anaweza kukaa hapo kwa siku kadhaa. Nina wasiwasi alimuua baada ya kugundua aliyekuwa mke wake na mama wa watoto wake alikuwa anarudi kutoka nje ya nchi”