Mwendokasi watangaza nafasi 360 za ajira
Sisti Herman
September 29, 2026
Share :

Kampuni ya usafiri ya Mofat imetangaza nafasi 360 za ajira, zikiwamo 200 za madereva wa Mabasi Yaendayo Kasi (BRT) na 160 za maofisa wa huduma kwa abiria.
Kwa nafasi za madereva, waombaji wanatakiwa kuwa na elimu ya msingi, kidato cha nne au cha sita, pamoja na leseni halali ya udereva Daraja C iliyothibitishwa na Jeshi la Polisi.
Mwombaji anatakiwa kuwa na cheti cha PSV kutoka Chuo cha Elimu ya Ufundi (Veta) au Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), cheti cha BRT kutoka NIT na uzoefu wa angalau miaka mitatu wa kuendesha mabasi au magari ya abiria.
Kwa upande wa maofisa wa huduma kwa abiria, kampuni imesema waombaji wanapaswa kuwa na cheti, stashahada au shahada katika fani husika kutoka taasisi inayotambuliwa.
Aidha, fani zinazokubalika ni pamoja na huduma kwa wateja, usafirishaji na ugavi, usimamizi wa biashara, mahusiano ya umma na nyingine zinazohusiana.
Mofat imesema mwisho wa kutuma maombi kwa nafasi za madereva ni Oktoba 9, 2026, huku waombaji wa nafasi za maofisa wa huduma kwa abiria wakitakiwa kuwasilisha maombi yao kabla ya Oktoba 5, 2026.





