Mwijaku kuhojiwa kisa sakata la mabinti wa chuo.
Joyce Shedrack
April 23, 2025
Share :
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amechapisha taarifa ya Wizara yake mtandaoni leo Jumatano Aprili 23, 2025 akieleza kuhusu muendelezo wa Mkasa wa video iliyoonekana Mtandaoni mwanzoni mwa wiki hii, ikionesha wanafunzi wa chuo Kimoja Jijini Dar Es salaam wakimshambulia na kumdhalilisha mwanafunzi mwenzao, wakidai kuwa wamebaini mwanafunzi huyo ana mahusiano na mwanaume aliyetajwa kwa jina moja la Mwijaku, akiwa ni mpenzi wa mmoja wa wanawake hao wawili.
Taarifa ya Waziri Gwajima imeweka wazi kuwa Mtu huyo aliyetajwa kwa jina moja la Mwijaku naye atafanyiwa mahojiano kwa mujibu wa sheria.
"Ndugu Wananchi, rejeeni taarifa yangu kwa umma ya tarehe 20 Aprili, 2025 kuhusu mada tajwa hapo juu. Jeshi letu la Polisi linaendelea kutimiza wajibu wake wa kisheria kuhusu kuwahoji wahusika wa tukio hilo.
Aidha, kwa upande mwingine, jamii nayo imeendelea kuhoji mbona aliyetajwa kuwa ni Mwijaku hakamatwi?
Ndugu Wananchi, napenda kuwahakikishia kuwa, Mwijaku aliyetajwa kwenye video za mgogoro wa mabinti hao, naye atahojiwa kwa mujibu wa Sheria na baada ya hapo, Wizara yangu itaona nini ifanye kuhusu mustakabali mzima wa maadili ya jamii na nafasi ya huyo Mwijaku na wengine wote wenye nafasi zenye kuchochea kasi ya athari chanya au hasi kwenye maadili ya jamii. Aidha, nawaomba tuwe watulivu na tuendelee kufuatilia taarifa za Jeshi letu la Polisi." Ameandika Mhe. Gwajima.