Mwili wa Pele kufukuliwa
Sisti Herman
January 24, 2024
Share :
Vyombo vya habari vya nchini Brazil vimeripoti mwanamke mmoja, Maria do Socorro Azevedo (60), ambaye anadai kuwa ni mtoto wa Mwanasoka Mkongwe, Marehemu Pele.
Mwanamke huyo amesema kuwa yeye ni mtoto wa nane wa Pele na anastahili kupata mali alizoziacha kwa ajili ya watoto wake na anataka mwili wa mwanasoka huyo ufukuliwe ili kufanyiwa vipimo vya DNA.
“Mama yangu hakumwambia Pele kuhusu ujauzito wake, niliomba vipimo mwaka 2019 lakini afya ya Pele pamoja na janga la corona vilisababishwa kukwama kwa mpango ule”
Taarifa kutoka Brazil, zinasema kuwa watoto wa Pele walikubali kufanyiwa vipimo vya DNA, ambavyo vilileta majibu hasi, hata hivyo mpango wa vipimo vingine unaandaliwa.
Naye, Edinho ambaye ni mmoja wa watoto wa kiume wa Pele anayesimamia mirathi amesema “tumeshafanya vipimo maabara, tukiwa na yeye na tumeshathibitisha kuwa huyo si dada yetu”
Pele,ambaye jina lake kamili ni Edson Arantes do Nascimento, alifariki dunia Desemba 2022, hata hivyo inasadikiwa kuwa katika wosia wake aliandika kuwa huenda akawa na mtoto wa nane , binti ambaye hawakuwahi kukutana.
Taarifa zinasema kuwa Pele alishakubali kufanyiwa vipimo hivyo, hata hivyo alifariki kabla ya kufanyika kwa zoezi hilo.
Mwanasheria anayemuwakilisha mjane wa marehemu amesema zoezi hilo halina busara na haliwezekani.
Utajiri wa Pele unakadiriwa kufikia kiasi cha pauni milioni 12, huku asilimia 30 ikiwa kwa ajili ya mjane, 60 kwa ajili ya watoto wake saba na asilimia 10 kwa ajili ya wajukuu zake wawili.