Nabi achanganyikiwa baada ya kupoteza ubingwa mechi ya mwisho.
Joyce Shedrack
June 15, 2024
Share :
Aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa klabu ya Yanga kwa sasa akikinoa kikosi cha AS Far Rabat ya Morocco Nasridine Nabi siku ya jana alipoteza ubingwa wa Ligi Kuu Nchini Morocco baada ya kuongoza ligi hiyo kwa takribani wiki 18 kabla ya Raja Club kumshusha kileleni mwa msimamo wiki mbili kabla ya ligi kutamatika wakiwa na tofauti ya alama moja pekee jambo lililosababisha kusubiri mpaka mchezo wa mwisho kuamua bingwa wa Ligi.
As Far Rabat ya Nabi walikuwa wanahitaji kushinda mchezo wao wa mwisho dhidi ya FUS Rabat huku wakiiombea Raja Club kupoteza ugenini dhidi ya Mouloudia Oujda ili watangazwe kuwa mabingwa, jambo lililoshindikana kutokana na kichapo walichokigawa Raja Club cha goli 3-0 na AS Far Rabat kupata ushindi wa 2-0 ambao haukuwawezesha kuwa mabingwa.
Raja Club imemaliza nafasi ya kwanza ikiwa na alama 72 na As Far Rabat imesalia nafasi ya pili kwa alama 71.
Kocha Nasridine Nabi alionekana kuwa mwenye huzuni kubwa baada ya michezo hiyo kutamatika.
Huwenda huo ukawa mchezo wa mwisho kwa Nabi Nchini Morocco kabla ya kutimkia Kaizer Chiefs inayotajwa tayari imemalizana naye kwa ajili ya kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo msimu ujao.