Nchi hizi 5 Afrika mafuta huuzwa kwa bei ya Chapati
Eric Buyanza
May 21, 2026
Share :

Wakati wananchi wa Tanzania na Kenya wakiendelea kulalamikia kupanda kwa bei ya mafuta kuanzia mwezi April na sasa Mei mwaka huu, baadhi ya mataifa ya Afrika bado yanaendelea kuuza mafuta kwa bei ya chini sana kulinganisha na wastani wa dunia.
Wakati Afrika Mashariki ikiendelea kubeba gharama hizo, kuna mataifa ambayo bado wananchi wake wananunua mafuta kwa bei ya chini sana kutokana na uzalishaji mkubwa wa mafuta, ruzuku za serikali na sera maalum za nishati.
Bei hizi za chini zinaweza kulinganishwa na bei kununua chapati moja ama mbili kulingana na bei ya chapati na ukubwa wake katika nchi za Afrika.
5. Sudan - Dola 0.700 kwa lita
Licha ya migogoro ya kisiasa na vita vya ndani, Sudan bado imo kwenye orodha ya mataifa yenye mafuta ya bei nafuu zaidi Afrika. Hii ni kutokana na uwepo wa uzalishaji wa mafuta katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo pamoja na mifumo ya udhibiti wa bei.
4. Misri - Dola 0.454 kwa lita
Misri imeendelea kuwa miongoni mwa mataifa yenye mafuta ya bei nafuu Afrika licha ya changamoto za kiuchumi zinazowakabili wananchi wake. Serikali ya Cairo imekuwa ikiingilia mara kwa mara sekta ya nishati ili kuzuia bei kupanda kwa kasi kubwa.
3. Algeria - Dola 0.355 kwa lita
Algeria ni moja ya mataifa makubwa zaidi ya mafuta na gesi katika eneo la Afrika Kaskazini. Uchumi wa taifa hilo unategemea kwa kiwango kikubwa mauzo ya mafuta na gesi asilia kwenda Ulaya.
2. Angola - Dola 0.327 kwa lita
Angola ni moja ya wazalishaji wakubwa wa mafuta katika eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara. Taifa hilo huzalisha zaidi ya mapipa milioni moja ya mafuta kwa siku, jambo linaloliwezesha kuwa na uwezo mkubwa wa kudhibiti bei za ndani.
1. Libya - Dola 0.024 kwa lita
Libya ndiyo nchi yenye mafuta ya bei ya chini zaidi Afrika na hata duniani kwa sasa. Bei hiyo ni ndogo sana kiasi kwamba lita moja ya mafuta nchini humo ni chini ya hata maji ya kunywa katika baadhi ya mataifa ya Afrika.
Sababu kubwa ni kwamba Libya ina moja ya akiba kubwa zaidi ya mafuta duniani. Taifa hilo lina zaidi ya mapipa bilioni 48 ya akiba ya mafuta yaliyothibitishwa, kiwango kinacholiweka miongoni mwa nchi 10 duniani zenye mafuta mengi zaidi.
BBC





