Ndege ya kivita ya Marekani yadunguliwa na Iran
Eric Buyanza
April 4, 2026
Share :

Iran imesema imedungua ndege ya kijeshi ya Marekani chapa A-10 karibu na mlango-bahari wa Hormuz, ikiwa ndege ya pili inayodai kuilenga katika muda wa siku moja. Rubani mmoja ameokolewa huku Tehran ikimsaka wa pili.
Vita kati ya Marekani, Israel na Iran vimeingia hatua mpya ya hatari baada ya ripoti kueleza kuwa ndege mbili za kijeshi za Marekani zimeanguka katika siku moja ndani na karibu na eneo la Ghuba.
Kwa mujibu wa ripoti hizo, ndege ya kwanza aina ya F-15E Strike Eagle ilidunguliwa juu ya ardhi ya Iran, huku ndege ya pili aina ya A-10 Warthog nayo ikiripotiwa kuanguka katika eneo la Ghuba, karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz.
Taarifa za awali zilisema mhudumu mmoja wa ndege ya F-15E aliokolewa akiwa hai, wakati operesheni ya kumtafuta mhudumu mwingine iliendelea chini ya mazingira hatari ya kivita.
Ndege ya A-10 Warthog, ambayo awali ilitajwa kutumiwa kushambulia meli za Iran katika Mlango wa Hormuz, iliripotiwa pia kuanguka Ijumaa, ingawa maelezo kamili ya tukio hilo hayakuwekwa wazi mara moja.
Kwa jumla, tukio hilo limeongeza wasiwasi mkubwa kuhusu uwezo wa Iran kuathiri moja kwa moja operesheni za Marekani angani, pamoja na kuonyesha kuwa vita hii sasa imepanuka zaidi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.
DW





