Netflix yashitakiwa kwa kuwachunguza watumiaji wake, ikiwemo watoto
Eric Buyanza
May 12, 2026
Share :

Jimbo la Texas nchini Marekani limefungua kesi dhidi ya kampuni ya Netflix, likiiweka katika tuhuma nzito za kukusanya na kutumia taarifa ama data za watumiaji wake, ikiwemo watoto bila ridhaa yao ya wazi, na baadaye kutumia taarifa hizo kwa malengo ya kibiashara na uboreshaji wa huduma zake.
Kesi hiyo, iliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Texas Ken Paxton, inadai kuwa Netflix imekuwa ikikusanya mabilioni ya taarifa kuhusu tabia za watumiaji wake. Taarifa hizo ni pamoja na kile wanachotazama, muda wanaokaa kwenye maudhui, na jinsi wanavyoingiliana na mfumo wa jukwaa hilo.
"Kila kinachofanywa na kwenye jukwaa hili kinageuzwa kuwa data inayoweza kumuanika mtumiaji," ofisi ya mwanasheria huyo imesema.
Netflix imekanusha vikali madai hayo, ikisema kesi hiyo haina msingi na inategemea taarifa zisizo sahihi na zilizopotoshwa. Kampuni hiyo imesisitiza kuwa inazingatia sheria za ulinzi wa data katika maeneo yote inakofanya kazi na kwamba inaheshimu faragha ya watumiaji wake.
"Kwa heshima ya jimbo kubwa la Texas na Mwanasheria Mkuu Paxton, kesi hii haina msingi na inategemea taarifa zisizo sahihi na zilizopotoshwa," msemaji wa Netflix aliiambia shirika la habari.
“Netflix inachukulia kwa uzito faragha ya watumiaji wetu na inazingatia sheria za faragha na ulinzi wa data kila mahali tunapofanya kazi.”
BBC





