Ngome yatetea ubingwa wa klabu bingwa ya ngumi taifa Tanga
Eric Buyanza
August 31, 2026
Share :

Timu ya ngumi ya Ngome JWTZ imefanikiwa kutetea ubingwa wa Mashindano ya Klabu Bingwa ya Taifa ya Ngumi Tanga 2026, baada ya kuongoza kwa jumla ya medali 6 za dhahabu, dhidi ya 5 za MMJKT.
Medali hiyo moja ya ziada ya dhahabu imeiwezesha Ngome kuwatangulia wapinzani wao wa jadi, MMJKT, na kutetea ubingwa walioutwaa mwaka 2025.
Katika nafasi za juu, MMJKT imemaliza mshindi wa pili, ikifuatiwa na Magereza katika nafasi ya tatu, huku Tanga ikimaliza nafasi ya nne.
Mashindano hayo yaliyofanyika Tanga yalishirikisha jumla ya vilabu 15 kutoka maeneo mbalimbali nchini, katika kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa wa Taifa.
Baada ya kumalizika kwa mashindano hayo, benchi la ufundi litafanya tathmini ya ushindani na viwango vya mabondia kwa lengo la kuunda na kuimarisha Timu ya Taifa kuelekea mashindano makubwa yajayo, ikiwemo Mashindano ya Ubingwa wa Afrika Kinshasa 2026, mashindano ya kufuzu Michezo ya Olimpiki Los Angeles 2028 kwa ngazi ya Afrika na dunia mwaka 2027, pamoja na Michezo ya Afrika 2027.





