Ni uzushi, Bony Mwaitege hajafariki
Sisti Herman
July 22, 2024
Share :
Msanii wa nyimbo za Injili, Bonny Mwaitege amesikitishwa na taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo kumezuka uvumi kuwa amefariki kwa ajali.
Akizungumza leo Jumatatu Julai 22, 2024 alipotafutwa na waandishi kuhusiana na taarifa hizo amesema kuwa yeye ni mzima wa afya na amesikitishwa na uzushi huo unaosambazwa mitandaoni.
"Aise pole sana, mimi ni mzima wa afya njema wala sijafa. Huu uzushi tu wa watu ukweli nimesikitika sana, maana nimeanza kupigiwa simu na watu kutokea Nairobi na Dar na mikoa mingine, hii ni mbaya sana. Hapa sasa hivi nipo njiani naelekea Nairobi kwenye kazi za injili, Mungu ni Mwema," amesema Mwaitege akiongea na mwandishi wa gazeti la Mwananchi.
Alipoulizwa iwapo uzushi huo kuwa ametengeneza kiki, amesema sio kiki kwani kwa hatua aliyopo sio wa kutaka kufanya kitu atumie kiki.
"Kwanini nifanye kiki? Yaani kiki ndio nijiue mwenyewe? Kwa hatua niliyofikia ya kazi ya sanaa yangu sio ya kufanya kiki ndio nifanye kitu," amesema Mwaitege.
Mwimbaji huyo amewahi kutamba na nyimbo nyingi zikiwemo Safari Bado, Dunia Dunia, Acha Nizaliwe, Bado Nampenda, Mke Mwema, Sisi Sote, Imba, Mama na Neema Imenibeba na nyingine.