Niliingizwa mjini na Arteta – Willian afichua kilichomponza
Eric Buyanza
October 7, 2026
Share :

Kiungo mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil, Willian, amefunguka na kukiri kuwa uamuzi wake wa kuondoka Chelsea na kujiunga na Arsenal mwaka 2020 lilikuwa kosa kubwa zaidi katika maisha yake ya soka, huku akifichua jinsi ahadi kubwa kutoka kwa kocha Mikel Arteta zilivyomponza.
Katika mahojiano ya hivi karibuni kwenye kipindi cha 'The Obi One Podcast', Willian alifichua undani wa jinsi Arsenal walivyomshawishi akatae ofa ya Chelsea na kuvuka upande wa Kaskazini mwa London.
"Nilipozungumza na Arteta na Edu (Mkurugenzi wa Ufundi wa Arsenal), waliniambia: 'Tunakuhitaji uje hapa, Utakuwa mhimili wetu....Tunataka kukupa funguo za klabu ili uwe kiongozi wa mradi huu mpya,'" alieleza Willian.
Ahadi hizo, zikiambatana na ofa ya mkataba wa miaka mitatu ambao Chelsea waligoma kumpa kutokana na umri wake wa miaka 32 wakati huo, ndivyo vilivyomfanya kusaini makubaliano na Washika Bunduki hao wa jiji la London.
Hata hivyo, mambo hayakwenda kama alivyotarajia. Willian alikiri kuwa mazingira na mfumo wa Arsenal haukumpa furaha kabisa, jambo lililomfanya aanze kujuta mapema sana.
"Baada ya miezi mitatu tu pale Arsenal, nilimpigia simu wakala wangu na kumwambia: 'Tafadhali, fanya kila unachoweza, nataka kuondoka hapa,'" alifichua nyota huyo.
Kutokana na kukosa amani ya nafsi, kiwango cha Willian kiliporomoka vibaya mno ambapo alifanikiwa kufunga bao 1 pekee katika mechi 37 alizocheza chini ya Arteta. Hali hiyo ilimfanya kuchukua uamuzi wa kipekee wa kuomba mkataba wake wa pauni 240,000 kwa wiki uvunjwe ili aondoke bure kurejea nchini kwao Brazil kujiunga na Corinthians, akitosa mamilioni ya fedha kwa ajili ya kutafuta furaha yake.
Willian ameweka wazi kuwa kama angekuwa na uwezo wa kurudisha nyuma muda, asingewahi kuondoka Chelsea ambako alicheza mechi 339, akifunga mabao 63 na kushinda mataji mawili ya Premier League, FA Cup, na Europa League.





