Nyuki wazua taharuki baada ya kuvamia shule Morogoro
Eric Buyanza
February 11, 2026
Share :

Masomo katika Shule ya Msingi Lukobe yameahirishwa kwa muda kufuatia tukio la kuvamiwa na kundi la nyuki majira ya asubuhi, hali iliyosababisha taharuki kubwa miongoni mwa wanafunzi na walimu. Katika tukio hilo, zaidi ya wanafunzi 11 pamoja na mwalimu mmoja walijeruhiwa baada ya kushambuliwa na nyuki hao.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mohamed Mangu, amesema nyuki hao walionekana kwa mara ya kwanza takribani siku nne zilizopita wakiwa wamekaa juu ya tanki la maji lililopo katika eneo la shule.
Uongozi wa shule ulijaribu kuziba njia waliyokuwa wakitumia, lakini juhudi hizo hazikuzuia hatari iliyojitokeza asubuhi ya leo, ambapo nyuki hao waliibuka kwa wingi na kuanza kushambulia wanafunzi waliokuwa wakiendelea na shughuli za usafi wa mazingira.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Sajenti Alexander Makuluni kutoka Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji amesema kuwa walipokea taarifa na kufika shuleni hapo haraka, ambapo wamefanikiwa kuwadhibiti nyuki hao kwa kiasi kikubwa.
Amesema nyuki hao tayari walikuwa wameanza kujenga makazi yao katika eneo hilo, na ametoa wito kwa walimu na wananchi kwa ujumla kutoa taarifa mapema pindi wanapoona dalili za uwepo wa makundi ya nyuki ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.
Kwa upande wa huduma za afya, Kaimu Mganga Mfawidhi wa zahanati ya lukobe, Judith Ntanyinya, amethibitisha kupokea wanafunzi 11 pamoja na mwalimu mmoja wakiwa na majeraha ya kung’atwa na nyuki.
Amesema mwalimu huyo amelazwa katika wodi ya wagonjwa kwa uangalizi zaidi kutokana na hali aliyofikishwa nayo, huku wanafunzi wengine wakipatiwa matibabu na kuruhusiwa kurejea majumbani kwao.
Naye Chiku Mussa Gaudence, mmoja wa wanafunzi walioshambuliwa, amesema kuwa tukio hilo lilitokea wakati walipokuwa wakifanya usafi wa asubuhi.
Ghafla waliona kundi kubwa la nyuki likiwajia kwa kasi na kuanza kuwashambulia, hali iliyowalazimu kukimbia hovyo kutafuta msaada.
Tukio hilo limeibua tahadhari kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua za haraka pindi viashiria vya hatari kama uwepo wa makundi ya nyuki vinapoonekana katika maeneo ya mikusanyiko ya watu, hususan shuleni.
@habarimorogoro





