Nyumba ya Rihanna yashambuliwa kwa risasi akiwa ndani.
Joyce Shedrack
March 9, 2026
Share :
Polisi wa Los Angeles nchini Marekani wanafanya uchunguzi baada ya nyumba ya Rihanna iliyopo Beverly Hills kushambuliwa kwa risasi Siku ya Jumapili.
Tukio hilo linaripotiwa kutokea majira ya saa 7 mchana kwa saa za huko, ambapo mshukiwa alifyatua takribani risasi 10 kutoka ndani ya gari lililokuwa upande wa pili wa barabara karibu na jumba hilo.
Maafisa wa polisi wanasema risasi moja ilipenya ukuta wa nyumba hiyo, ambayo Rihanna anaishi pamoja na mwenzi wake, rapa A$AP Rocky, pamoja na watoto wao.
Polisi wamethibitisha kuwa Rihanna alikuwa ndani ya nyumba wakati wa tukio, lakini hakupata majeraha. Hadi sasa, mwimbaji huyo bado hajatoa tamko rasmi kuhusu tukio hilo.
Kwa mujibu wa polisi, mshukiwa ni mwanamke mwenye umri wa takribani miaka 30 ambaye alikimbia kutoka eneo la tukio mara baada ya kufyatua risasi.
Wachunguzi wanaamini kuwa mshukiwa alifyatua risasi kadhaa kuelekea nyumba hiyo akiwa ndani ya gari, ingawa hadi sasa sababu ya shambulio hilo bado haijajulikana.
Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, huku polisi bado hawajatoa jina la mshukiwa hadharani.





