Okwi atangaza rasmi kustaafu kucheza soka la ushindani
Sisti Herman
August 4, 2026
Share :

Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Uganda na gwiji wa klabu ya SIMBA SC, Emmanuel Arnold Okwi, ametangaza rasmi kustaafu kucheza soka la kulipwa, akifunga ukurasa wa safari yake ya miaka mingi iliyogubikwa na mafanikio, uzalendo na kumbukumbu zisizosahaulika.
Kupitia taarifa aliyoiandika kwa hisia, Okwi amesema uamuzi huo ni miongoni mwa maamuzi magumu zaidi kuwahi kufanya maishani mwake, akieleza kuwa soka halikuwa ajira tu bali lilikuwa ndoto, shauku na kusudi ambalo amebahatika kuliishi kila siku.
Mshambuliaji huyo amesema kuivaa jezi ya timu ya taifa ya Uganda (Uganda Cranes) ilikuwa heshima kubwa zaidi katika maisha yake ya soka, huku kuaminiwa kuvaa kitambaa cha unahodha kukibaki kuwa moja ya mambo atakayoyathamini milele.
Okwi pia ametoa shukrani kwa klabu zote alizowahi kuzitumikia, makocha waliompa nafasi, wachezaji wenzake waliokuwa bega kwa bega naye pamoja na wapinzani waliomsaidia kukua na kuwa mchezaji bora zaidi.
Aidha, hakuwasahau mashabiki ambao amesema wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio yake, wakimpa nguvu katika nyakati za furaha na hata kipindi kigumu, jambo ambalo amesema hatalisahau kamwe.
Hata hivyo, Okwi ameweka wazi kuwa ingawa amestaafu kucheza soka, safari yake ndani ya mchezo huo haijafikia mwisho. Amesema ataendelea kulitumikia soka kwa njia nyingine, akilenga kuchangia maendeleo ya mchezo huo pamoja na kuhamasisha na kukuza kizazi kipya cha wachezaji.
"Ninafunga ukurasa huu nikiwa na fahari kubwa, shukrani na kumbukumbu nyingi nzuri. Soka limenipa zaidi ya nilivyowahi kufikiria, na kwa hilo nitaendelea kushukuru milele," amesema Okwi.
Kwa kauli hiyo, Emmanuel Okwi anaaga rasmi maisha ya uwanjani akiwa mmoja wa wachezaji waliolihudumia taifa la Uganda kwa kujituma na kuwa miongoni mwa nyota waliotoa mchango mkubwa katika soka la Afrika Mashariki.
**Mwisho wa ukurasa mmoja, mwanzo wa mwingine.** Huo ndio ujumbe ambao Emmanuel Okwi ameacha kwa mashabiki wake na familia ya soka baada ya kutangaza kustaafu rasmi kucheza soka la kulipwa.






