Pacha waoa pacha wenzao katika harusi ya kipekee Nigeria
Eric Buyanza
June 23, 2026
Share :

Wakati wageni walipokusanyika katika kanisa jijini Ibadan kusini-magharibi mwa Nigeria mwishoni mwa wiki, walijua walikuwa wakishuhudia tukio la kipekee.
Ndugu mapacha wawili wa kiume, Taiwo na Kehinde Oguntoye, walifunga ndoa na dada mapacha wawili wa kike, Taiwo na Kehinde Adediran, katika sherehe ya pamoja iliyojaa furaha.
Jamii ya Wayoruba, ambao ni wengi eneo la kusini-magharibi mwa Nigeria, inajulikana kwa kuwa na kiwango cha juu cha kuzaliwa kwa mapacha. Hata hivyo, si jambo la kawaida kuona jozi mbili za mapacha wakifunga ndoa kwa wakati mmoja.
Akizungumza siku ya harusi yake, Taiwo Oguntoye alisema:
"Tunawafahamu mapacha wengi, lakini ndoa hii inaonekana kama ilipangwa na Mungu. Siku zote tumekuwa na ndoto ya kuoa mapacha."
Aliongeza kuwa yeye na mke wake wanaomba wapate watoto mapacha katika watoto wao wa kwanza na wa pili, kwani hilo ndilo tamanio lao kubwa.
Katika utamaduni wa Wayoruba, mapacha huchukuliwa kuwa baraka maalumu. Majina yao pia hupewa kwa kufuata mila za kitamaduni. Mtoto anayezaliwa kwanza huitwa Taiwo, ambalo maana yake ni "yule anayekwenda kuujaribu ulimwengu", huku anayezaliwa baadaye akiitwa Kehinde, likimaanisha "yule aliyekuja baada yake".
Tukio hilo limevutia watu wengi kutokana na nadra yake na umuhimu wake wa kitamaduni katika jamii ya Wayoruba.
BBC





