Papa Francis, Rais Samia wakutana Vatican
Eric Buyanza
February 12, 2024
Share :
Rais Samia Suluhu Hassan, jana Februali 11, mwaka huu ameanza ziara yake Vatican kwa mwaliko wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis.
Papa Francis alimpokea Rais Samia mara baada ya kuhudhuria misa takatifu katika Kanisa la Mtakatifu Peter (St Peter’s Basilica).
Ziara hiyo itakuwa ya siku mbili, yaani Februari 11 na 12 na Febrauri 13 Rais atawasili Norway kwa ziara nyingine ya siku mbili.
Jana, Februari 11, 2024, ambayo ilikuwa siku ya maadhimisho ya miaka 95 ya uhuru wa Dola ya Vatican. Februari 11, 1929, aliyekuwa Mfalme wa Italia, Victor Emmanuel III na Papa Pius XI, walisaini Mkataba wa Lateran, ulioitambua Vatican kuwa ni Kiti Kitakatifu (The Holy See).
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, Rais Samia akiwa Vatican, atakuwa na mazungumzo na Baba Mtakatifu Papa Francis pamoja na Katibu wa Vatican, Pietro Parolin.
Alisema uhusiano kati ya Tanzania na Vatican ulianza miaka ya 1960 wakati ambapo Vatican ilianzisha Ubalozi wake hapa nchini.
Tangu wakati huo Vatican kupitia Kanisa Katoliki imekuwa mstari wa mbele katika kujishughulisha na masuala ya kiroho, amani, elimu na program za afya.