Pep na Diniz, ilikua mechi yenye ladha tofauti karne hii
Sisti Herman
December 25, 2023
Share :
Tarehe 22 mwezi wa 12 mwaka 2023 inaweza kuwa siku bora kwa wanazi wa mbinu za soka pale Manchester City walipotwaa ubingwa wa dunia ngazi ya vilabu jana baada ya kushinda magoli 4-1 dhidi ya Fluminense kwenye mechi ambayo inaweza kutajwa kama mechi bora ya karne kwasababu tofauti huku sababu kubwa ni kuwakutanisha makocha ambao hutambulisha falsafa mbili tofauti za mbinu za uchezaji wa soka, Pep Guardiola anayeaminika kuwa bora zaidi kwenye falsafa ya “Positional Play” na Fernando Diniz anayeaminika kuwa bora kwenye falsafa ya “Functional Play”
Positional Play (Juego de posicion)
Ni style ya uchezaji ambayo timu ikishambulia, wachezaji hujipanga uwanjani kulingana na maeneo maalum ambayo hupimwa na kugawa uwanja na kupata wastani mzuri wa marefu na mapana, ambayo;
- Tabia yake kuu ni mchezaji hufuatwa na mpira kwenye nafasi na sio mchezaji kuufuata mpira
- Kocha anayetumia zaidi style hii ni kwenye ubora ni Pep Guardiola
- Wakosoaji wa style hii hulalamika kuwa ni style isiyowapa wachezaji uhuru kuonyesha ubunifu kutokana na uwezo wao kiufundi (limited)
- - Wakosoaji wa style hii wanasema ni style ambayo huwafanya wachezaji kuwa maroboti kwa majukumu ya kimbinu kuwabana kuonyesha uwezo wao kiufundi kwa uhuru
Functional Play (Dinizismo)
Ni style ya uchezaji ambayo timu ikishambulia, hujipanga uwanjani kwa kuufuata mpira ulipo, kujaa eneo hilo, kuwa pamoja wakiwa wengi kwenye eneo dogo ili kufaidiana kwa uwezo wao wa kiufundi
- Tabia yake kuu ni mchezaji kuufuata mpira na sio mpira kumfuata mchezaji
- Kocha anayetumia zaidi style hii kwenye ubora ni Fernando Diniz
- Wakosoaji wa style hii hulalamika kuwa hutegemea zaidi uwezo wa wachezaji kiufundi kuliko mbinu za kocha kiasi kwamba wachezaji hutumia nishati kubwa kwa kukimbia kwenye maeneo
- Ni style ambayo wachezaji wabunifu huwa huru kuonyesha ubunifu wao kwa uhuru zaidi (not limited)
DAKIKA 90 NA VITA YA MBINU
Kwenye jicho la mbinu ni mchezo ulioamuliwa na style za uchezaji za makocha hawa na sio miundo au mifumo ya uchezaji, mifumo ilisindikiza tu sherehe hizo
Mifumo ilikuwaje?
Pep Guardiola
Mhispaniola huyu hutumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao hunyumbulika kwenye miundo tofauti kulingana na mahitaji ya wakati husika uwanjani, mfano hutumia;
• 3-2-2-3 pindi timu yake inapokuwa na mpira ambapo mfumo hunyumbilika kwenye maeneo matatu tofauti, kwenye mstari wake wa mabeki, kati ya wanne walioanza (4-2-3-1) yaani Dias,Stone, Walker na Ake, mmoja Stone wao husogea mbele usawa wa kiungo wa kati, Rodri na watatu kubaki nyuma, wakati huo pia kiungo aliyekuwa usawa Rodri (double pivot kwenye 4-2-3-1) yaani Rico Lewis husogea mbele usawa wa kiungo mshambuliaji wa kati Foden na kutengeneza viungo wanne kwenye muundo wa box (2-2) nyuma ya washambuliaji watatu, baada ya viungo washambuliaji wa pembeni Grealish na Bernado kusogea kwenye mapana ya uwanja usawa wa mshambuliaji wa kati Julian Alvarez.
• 4-4-2 pindi timu isipokuwa na mpira hurejea kwenye muundo huu, Stone hurudi usawa wa mabeki wenzake kuwa wanne nyuma kwenye mstari wa mwisho wa uzuiaji mbele ya kipa, Rico Lewis hurudi usawa Rodri (Double Pivot), Grealish na Bernado husogea usawa wa viungo wawili wa kati na kukamilisha mstari wa pili wa uzuiaji wenye watu wanne huku mstari wa mbele wa uzuiaji ukiwa na mshambuliaji wa kati Alvarez ambaye huungana na kiungo mshambuliaji wa kati Foden kukamilisha idadi ya watu wawili mbele. Muundo huu pia huweza kuwa 4-4-1-1 au 4-2-3-1.
Fernando Diniz
Mbrazil huyu hutumia muundo wa 4-2-3-1 ambao hunyumbulika kwenye miundo tofauti kulingana na mahitaji ya wakati husika uwanjani, mfano;
• 4-5-1 pindi wanapozuia kwenye theluthi zao mbili za mwanzo za uwanja lakini City wakianzisha shambulizi kuanzia kwenye theluthi yao ya kwanza, Fluminense hulazimisha mashambulizi ya City kupita pem,beni upande mmoja na kuzuia kwa kila mtu kuwa na mtu wake kwa wale wachezaji wa City wanaoweza kupokea mpira kwenye upande huo, Mshambuliaji wa kati wa Fluminense dhidi ya beki wa kati mwenye mpira, winga wa Fluminense dhidi ya beki wa pembeni wa City, kiungo mshambuliaji wa fluminense dhidi ya kiungo wa kati wa City (Man Marking)
•Wakiwa na Mpira Fluminense hawakuwa na mfumo, hujaa wote eneo lenye mpira, hutengeneza muundo ambapo huweza kutoa mpira eneo lenye presha kubwa ya City waliyoiita na kuvunja mistari ya uzuiaji kwa muunganiko wa wachezaji wao ambao hutegemeana kiufundi
Style za uchezaji zilikuwaje?
Fluminense
Wakiwa na mpira
Huanza kujenga mashambulizi kuanzia kwenye lango lao (Building from back), wakitegemea City wawafuate (attracting pressure), baada ya kukaribisha shinikizo la City huanza kuivuka pressing structure ya City kwa pasi fupi, wakiwa karibukaribu sana wakiivunja mistari ya City huku wakitegemea mambo matatu;
• Faida ya idadi (Numerical Superiority); muundo wa kuzuia wa City (pressing structure) kwenye shape yao ya 4-2-3-1 wakizuia huwa na watu wachache dhidi ya muundo wa kujenga shambulizi wa Fluminense (Build up structure) ambapo huwa na watu zaidi ya watatu kwenye mstari wa nyuma, kwahiyo mstari wa kwanza wa uzuiaji wa City dhidi ya mstari wa kwanza wa ujenzi wa shambulizi wa Fluminense huwa (3v1)
• Faida ya uwezo wa wachezaji kiufundi (Qualitative Superiority); uwezo wa kiufundi wa wachezaji wengi wa Flumenense na kuwa kwao karibu karibu hufaidiana kwenye ujenzi wa mashambulizi kutopoteza mpira, kuna nyakatoi wachezaji wenye uwezo wa kumiliki mpira bila kupoteza pindi wanaposhinikizwa kama Ganso na Marcelo (Press Resistant) hushuka hadi eneo lenye presha ya City na kutoka kwa uhuru
Baada kutoka eneo lenye presha kubwa Flumenense hufaidika na kuwavuta City kwenye upande moja la uwanja wakiwa wengi (tilting) na kuuacha upande mwingine na watu wasiozidi wawili ambao wana uwezo mkubwa dhidi ya mpinzani mmoja (1v1) na hao huwaita Difensive Diagonal, hutumia pasi ndefu kwa haraka kwenye upande waliouacha ambao pia City huwa wameuacha na kufanya Switch Play kwa kupiga pasi ndefu na za haraka kwa huyo Difensive Diagonal ambaye mara nyingi ni beki wa pembeni Samuel Xavier kisha kuanza kuzithuru theluthi ya kati na ya mwisho ya uwanja
Wasipokuwa na Mpira
Fluminense wasipokuwa na mpira huzuia wakiwa wamefinya uwanja au kubana nafasi kati ya mchezaji na mchezaji kuwa ndogo huku wakiweka presha kwa eneo amchezaji wa City aliye na mpira kwenye kila theluthi;
• Wakizuia kuanzia theluthi ya mbele pindi City wakijenga shambulizi, wanachokifanya wao ni kulazimisha shambulizi liende pembeni upande mmoja, kisa hufanya Man marking kwa wachezaji wa upande huo wote na kuweka presha kwa mchezaji mwenye mpira
• Wakizuia kwenye theluthi ya katikati na kwao hujipanga na muundo wa 4-2-3-1, wachezaji hurudi kwenye nafasi zao, wakifinya uwanja katikati bila kuachinana nafasi kubwa kati yao huku wakiendelea kuweka presha kubwa kwa mchezaji mwenye mpira
Man City
Wakiwa na mpira
Man City wakiwa na mpira walijaribu kujenga mashambulizi ya pasi fupi kwenye muundo wa 3-2-2-3 kama walivyozoea lakini nyakati nyingi walikua kwenye pressure kubwa kutoka kwa Fluminence, lakini kwasababu ya Quality ya wachezaji walionao waliweza kuwa watulivu kwenye nyakati za presha na kuweza kufanya Build up zao kirahisi
• Kuna nyakati Fluminense waliachiana nafasi kubwa kati ya mtu na mtu pindi wanapozuia na Man marking, City waliweza kupita katikati yao hasa kumtumia Stone ambaye husogea nyuma ya mstari wa kwanza wa uzuiaji wa Fluminense na kuwa kama Free man au third man runners kwenye eneo la kiungo usawa wa Rodri (passing through)
• Kuna nyakati Fluminese waliacha nafasi upande mmoja wa uwanja pindi wanapolazimisha City kwenye upande mmoja, City waliweza kupita kwa pasi za juu kuhamisha upande hawa wakitegemea wachezaji wa pembeni kushambulia mapana ya uwanja kama Grealish na Bernado (Passing Around)
• Kuna nyakati Fluminense walisogea sana kwenye lango la City na kuacha nafasi kubwa nyuma yao, City walipiga pasi nyingi za juu kushambulia nafasi nyuma ya mstari wa ulinzi wa Fluminense huku silaha kubwa ikiwa Julien Alvarez kushambulia maeneo (Passing Over)
Wasipokuwa na mpira
Man City walianza kushinikiza kuanzia mbele kwa Fluminense ili kutunza muda na nafasi huku wakilazimika kwa kushawishiwa na namna Fluminense wanavyojenga shambulizi kuanzia kwenye lango lao wakijaribu kuhitaji kufaidika kama watazuia vuzuru kupokonya mpira na kushambulia kwa kujibu ambapo walizuia kwa mashinikizo na miundo tofauti kama;
• Shinikizo kubwa na muundo wa 4-2-3-1 wakizuia kwenye theluthi ya ujenzi wa mashambulizi ya Fluminense ili kufaidika na ukaribu wao na lango la wapinzani kwasababu ni kama Fluminense walikuwa wanacheza na shilingi karibu na tundo la choo.
• Shinikizo la kati na la chini na muundo wa 4-4-2 wakizuia kwenye theluthi ya kati na ya nyuma kwenye lango lao ili kutoachiana nafasi amvayo Flumeninse huweza kupita katikati yao, umoja ukiwa silaha kubwa.
MBINU ZA FLUMINENSE NA UTAMBULISHO WAO VILIVUTIA
Licha ya kufungwa mabao 4-0 na Man City, mashabiki wengi waliondoka na burudani iliyotokana na mbinu zinazotumiwa na kocha wa Fluminense Fernando Diniz ambazo hata Pep Guardiola alivutiwa nazo akikiri zina ule utambulisho wa soka la asili ya kibrazili ambao ulianza kupotea kutokana na namna mpira unavyozidi kubadilika kizazi hadi kizazi.
Hizi ni baadhi ya tabia zinazotambulisha mbinu za Diniz (DINIZISMO);
1. Apositional - Mpira wa sasa umekuwa ukichezwa kwa miundo maalum kwenye mifumo ambayo huwaongoza wachezaji kimajukumu na wakati mwingine huwanyima uhuru wa kufanya majukumu zaidi ya wanayohitajika kufanya kwenye mifumo lakini aina ya soka la Diniz huwafanya wachezaji kuwa huru kwasababu ni kama hawana muundo unaowalazimisha kuwepo kwenye maeneo ambayo hayawapi uhuru wa kufanya majukumu ya ziada.
2. Tilting - hii ni tabia ya wachezaji kucheza sana upande mmoja zaidi wa uwanja ili kuwa karibu karibu zaidi ili kufaidiana kwa uwezo wao wa kiufundi (combinations play)
3. Switch Play - hii hutokea pindi wanapokuwa eneo moja la uwanja, kukaribisha presha ya wapinzani, baada ya wapinzani kuwafuata eneo hilo wao kucheza pasi ndefu ambayo hutoa mpira eneo lenye presha kubwa na kupeleka eneo lenye presha ndogo ambalo liliachwa wazi na idadi ndo ya wachezaji, wasiozidi wawili
4. Difensive diagonal - staili ya Diniz ya wachezaji kuhamia upande mmoja wa uwanja na kuuacha upande mwingine ukiwa wazi huwa na tabia ya kuacha mmchezaji mmoja au wawili upande mmoja wa uwanja ambaye huwa na uwezo wa kushambulia nafasi kwa kasi, mzuri dhidi ya mpinzani mmoja au wawili (1v1) hao huitwa Difensive Diagonal.
5. Improvisation - hii hutokea pale wanapokuwa kwenye presha kubwa ya wapinzani, wachezaji hufanya vitu vilivyo nje ya mbinu kwakutumia maarifa na uwezo wao wa kiufundi kama kujaribu kukokota na kuchenga wachezaji zaidi ya wawili, hufanya hivi wakiwa na bima ya kuwa pamoja kwamba ikishindikana kwa umoja wao watapokonya mpira utakaopotea tena.
6. Versatility - staili ya Diniz huhitaji wachezaji kubadilishana sana nafasi uwanjani, kwasababu haina muundo (appositional) hutegemea zaidi uwezo wa wachezaji kiufundi (funtional play) hivyo wachezaji wengi huhitajika kuwa na uwezo wa kiufundi kucheza nafasi tofauti
7. Pressure - staili ya Diniz ya kuzuia huwa ya kutumia shinikizo kubwa kwa wapinzani ili wafanye makosa na wao wayatumie kuwashambulia.
MAPUNGUFU YA STAILI YA FLUMINENSE AMBAYO MAN CITY WALIYATUMIA KUWAADHIBU NI YAPI?
Mapungufu ya Fluminense mengi ya kimbinu yalitokea kwenye ubora wa mbinu zao, ina maana Guardiola alifanya tathmini nzuri na kutengeneza madhaifu kutoka kwenye ubora wao, mfano ni kama;
• Fluminense waki attract pressure upande mmoja wa uwanja ili wa switch kwa difensive diagonal wao, City wanakuwa wameshafika kuzuia mpira usifike kwa Difensive Diagonal, hata bao la kwanza lilitokea hapo, Marcelo alijaribu kufanya switch play kabla mpira haujafika kwa winga wa kulia Nathan Ake akaunasa na kujibu shambulizi ambalo Alvarez alilimalizia vizuri
• Flumenense pia kuna nyakati wakizuia walikuwa wapo nyuma ya mpira wengi hasa wakiwa kwenye theluthi zao mbili za nyuma lakini wakawapa City muda na nafasi kidogo sana ya kuwa na mpira na City kwasababu wana wachezaji ambao wan ubunifu na bongo zinazofanya maamuzi haraka wakawaadhibu, mfano bao la pili, Fluminense wakizuia kwenye nusu yao walishindwa kuwapa City presha, Rodri akawa na muda na nafasi ya kufikiria na kumuona Foden ameji position eneo zuri, akapiga pasi mpenyezo ambayo ilimfikisha haraka mbele ya lango.
• Pia hata nyakati Flumenense wakizuia na presha kubwa bado kuna baadhi ya vitu vilikwama kutokana na ubora wa wachezaji wa City kwa utimamu wa mwili na umri mdogo hasa nyakati za mipira ya kupambani juu na ya pili mingi City walifaidika nayo pindi wanapochagua kupita juu, mfano bao la tatu, Kovacic alishinda mpira wa kugombani na kufaidika nao kusogea nao kwenye lango la Fluminense na kutengeneza bao lililofungwa na Foden
• Pia tatizo la utimamu wa mwili na umri mkubwa wa wachezaji wa Fluminense ulishindwa kuwapa nishati ya kucheza kwa staili yao kwa dakika zote, kuna nyakati walizuia wakiwa wazi sana, mfano bao la nne la City, walizuia kwa nishati na nidhamu ndogo ya kubana uwanja hadi Nunez akatengeneza bao lilifungwa na Alvarez ambaye alikuwa huru kiasi.
Yote kwa Yote ni mechi iliyowakutanisha makocha wenye falsafa tofauti ambao wanatajwa kuwa vinara wa kutambulisha falsafa hizo ulimwenguni kuliko wengine wote ambao wanaziwasilisha kwenye jukwaa kubwa kama kombe la dunia la vilabu, NI MECHI BORA YA KARNE