Pesa anazomiliki Ronaldo zinatokana na kazi ngumu - Toni Kroos
Eric Buyanza
October 20, 2026
Share :

Kiungo wa zamani wa Real Madrid na timu ya taifa ya Ujerumani, Toni Kroos, ameweka wazi siri kubwa inayomfanya mshambuliaji Cristiano Ronaldo kuendelea kuwa kileleni mwa ulimwengu wa soka kwa miaka mingi.
Akizungumza na vijana wanaochipukia katika akademia yake ya soka ya Toni Kroos Academy iliyopo Madrid, Kroos amewataka wachezaji hao wadogo kutazama upande wa pili wa maisha ya Ronaldo nje ya uwanja, akisisitiza kuwa mafanikio hayaji kwa bahati mbaya.
Kroos, ambaye alikuwa jirani wa karibu wa nyumba ya Ronaldo wakati wakicheza pamoja nchini Uhispania, alisimulia jinsi nidhamu ya CR7 ya kuwahi mazoezini ilivyomshangaza kila siku.
"Unapaswa kila wakati kujitahidi kuwa bora zaidi. Mfano ninaoupenda zaidi ni Cristiano Ronaldo," alisema Kroos. "Kila mara nilipokuwa nikienda mazoezini, gari lake lilikuwa tayari limefika. Na kila nilipokuwa nikiondoka mazoezini, gari lake bado lilikuwa liko hapo."
Kiungo huyo mstaafu aliongeza kuwa kile ambacho Ronaldo amekipata maishani kimetokana na "juhudi kubwa na tamaa isiyoisha ya mafanikio."
Kroos alitumia fursa hiyo kuwapa ukweli vijana hao kuhusu taswira ya nje ya mastaa wa soka, akisema kuwa mashabiki wengi huvutiwa tu na matokeo ya mwisho bila kujua kazi kubwa inayofanyika gizani.
"Watu wengi wanachokiona ni kwamba anafunga mabao mengi na anaendesha magari ya kifahari. Mimi nilikuwa jirani yake, na ninaweza kusema kweli kwamba ana magari mengi mazuri—hata mimi nina moja (alicheka). Lakini yote hayo yamekuja kwa sababu ya kufanya kazi kwa bidii sana."





