Pitso na jeshi lake wapata dili Saudia
Joyce Shedrack
January 26, 2024
Share :
Kocha wa zamani wa klabu ya Al ahly ya Misri na Mamelod sundowns ya Afrika kusini Pitso Mosimane, raia wa Afrika Kusini amesaini mkataba wa muda mfupi na Klabu ya Abha inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia.
Pitso ametambulishwa Abha akiwa sambamba na wasaidizi wake wa benchi ufundi Maahier Davids (kocha msaidizi), Kabelo Rangoaga a.k.a KB (Kocha wa viungo), Musi Matlaba (Mtathmini wa viwango), Kyle Solomon (Mtathmini wa viwango), na kocha wa magolikipa Hamad Alyami wote wamesaini mkataba kuikinoa kikosi hiko cha Abha Club.
"Nina furaha kurejea katika ligi kuu ya Saudi Arabia, Abha Club imepanda ligi kuu ya Saudia Arabia haraka ukizingatia wamecheza ligi daraja la tatu misimu minne iliyopita, sasa klabu inapitia nyakati ngumu , nina heshima kwamba Rais na bodi wameniamini na kunipa jukumu la kuibakiza timu ligi kuu" alisema Kocha Pitso Mosimane baada ya kuukwaa mradi huo.
Hii si mara ya kwanza kwa kocha huyo kufundisha Saudi Arabia kwani msimu wa mwaka 2022/2023 aliifundisha Al ahli Saudi kabla ya kutimkia Falme za Kiarabu (UEA) kufundisha klabu ya Al wahda .
Pitso ana kibarua kizito cha kuinusuru timu hiyo isishuke daraja kwani Abha Club ipo nafasi ya 17 nafsi ya pili kutoka mwisho kwenye msimao wa Ligi Kuu Saudi Arabia ikiwa imecheza michezo 19 na kukusanya alama 14 pekee baada ya kushinda michezo 4 na kutoa sare katika mechi 2 .