POLISI WAFUTA MACHOZI YA SIMON: Ndoto yake ya elimu yafufuka
Eric Buyanza
September 2, 2026
Share :

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limemsaidia mwanafunzi Simoni Masanja, aliyekwama kuendelea na masomo ya Kidato cha Tano kutokana na kukosa mahitaji muhimu ya shule, kwa kumkabidhi vifaa mbalimbali vitakavyomwezesha kuanza masomo katika Shule ya Sekondari Lugugu, Mkoani Kigoma.
Msaada huo umekabidhiwa Septemba 1, 2026 katika Ofisi ya Polisi Mkoa wa Tabora na Mkuu wa Kitengo cha Polisi Wasaidizi kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Dkt. Debora Magiligimba, kwa kushirikiana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Twaha Lulengelule.
Msaada huo umetolewa baada ya kubainika kuwa wazazi wa mwanafunzi huyo, wanaoishi Kata ya Kalunde, Manispaa ya Tabora, hawakuwa na uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu ya shule tangu alipochaguliwa kuendelea na masomo ya Kidato cha Tano.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, SACP Dkt. Debora Magiligimba amesema hatua hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa Jeshi la Polisi katika kushirikiana na jamii, hususan kuwasaidia watoto na wanafunzi wenye uhitaji ili waweze kutimiza ndoto zao za kielimu.
Kwa upande wake, mwanafunzi Simoni Masanja amelishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada huo, akisema ndoto yake ya kuendelea na masomo ilikuwa mbioni kutoweka kutokana na ukosefu wa mahitaji muhimu ya shule. Ameahidi kutumia fursa hiyo kwa kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika masomo yake.
@polisi.tanzania





